MASHINDANO ya msimu huu ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN 2024) yametajwa kuwa bora zaidi kiushindani na wajumbe wa masuala ya kiufundi ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF TSG) na yameonyesha maendeleo makubwa kuliko yaliyopita.
Wajumbe hao, akiwemo Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ethiopia, Abraham Mebratu na mchezaji wa zamani wa Afrika Kusini, Mark Fish, walitoa tathmini hiyo wakiwa kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha NTV nchini Kenya.
Katika mahojiano hayo, walizungumzia mwenendo wa kiufundi wa hatua ya makundi na mashindano hayo yamejaa ubunifu wa kimbinu, ubora wa wachezaji na mbinu mpya za ufundishaji kutoka kwa makocha.
Fish alisema tofauti na mashindano yaliyopita, timu nyingi zimekuwa na uchezaji wa kushambulia zaidi, wakitumia mifumo ya kisasa na hata mabeki kushiriki kama viungo wa kati. Matokeo yake, mabao mengi yamefungwa (74) katika mechi 36, wastani wa mabao mawili kila mchezo.
Miongoni mwa mechi zilizovutia zaidi ilikuwa ushindi wa mabao 4-2 wa Burkina Faso dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, huku Sudan ikishinda kwa tofauti kubwa zaidi ya mabao 4-0 dhidi ya Nigeria kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Fish pia alisifu utofauti wa wachezaji akisema: “Wachezaji wamekuwa wakibadilika zaidi, wakifunga mabao mengi na kuonyesha mwelekeo mpya wa soka la Afrika. Ni jambo linalosisimua kwa mustakabali wa mchezo huu.”
Mebratu aliongeza, kasi ya mpira imeongezeka, huku timu zikibadilika haraka kati ya kushambulia na kujilinda. “Kuna maboresho makubwa hasa eneo la mashambulizi. Timu zinacheza kwa kasi na nidhamu kubwa,” alisema. Jambo jingine lililojitokeza ni ujasiri wa makocha kuwatumia wachezaji chipukizi, baadhi yao wakiwa na umri wa miaka 17 pekee. Vijana hao wameonyesha nidhamu ya kimbinu na ari kubwa.
Mwenendo wa wenyeji pia umepongezwa, kwani Kenya, Uganda na Tanzania zote zimefuzu hatua ya robo fainali. Kenya na Tanzania ziliibuka vinara wa makundi yao, huku Uganda ikitinga robo fainali baada ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Afrika Kusini.
Katika robo fainali, Kenya inakutana na Madagascar, Tanzania dhidi ya Morocco na Uganda wakivaana na mabingwa watetezi Senegal.