Geita. Serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa maabara ya kisasa ya utafiti wa madini mkoani Geita, itakayohudumia mikoa saba ya kimadini katika Kanda ya Ziwa ambayo ni Geita, Mbogwe, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Kahama na Mara.
Maabara hiyo inayotarajiwa kuwa kituo cha umahiri wa huduma za kimaabara inajengwa kwa gharama ya Sh3.5 bilioni na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Agosti 2026.
Waziri wa Madini, Antony Mavunde akizungumza baada ya kutembelea eneo la ujenzi lililopo Kata ya Kasamwa wilayani Geita.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo la ujenzi lililopo Kata ya Kasamwa wilayani Geita, Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema Serikali inajenga maabara tatu za kisasa katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Dodoma na Geta, lengo likiwa ni kuona sekta ya madini inakua kivitendo.
“Dodoma inajengwa maabara kubwa itakayotoa huduma bora Afrika Mashariki na kati na itakua inatoa huduma yenye ubora, Rais amedhamiria kuona sekta hii haikui kwa maneno tu, bali kwa vitendo na moja wapo ni kuiboresha sekta hii ya utafiiti ambayo ni moyo wa madini,” amesema Mavunde.
Kukamilika kwa maabara hiyo kutawaondolea wachimbaji wa madini adha ya kusafiri umbali wa zaidi ya saa nane kutoka Geita kwenda Dodoma kwa ajili ya vpimo vya kimaabara.
“Kwa sasa wachimbaji wanatembea zaidi ya saa nane kufika Dodoma kutafuta huduma, ukanda huu ndio unaoongoza kwa shughuli za madini hasa Mkoa wa Geita, huu ndio mkoa unaoongoza kwa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupita sekta ya madini,” amesema Mavunde.

Amesema katika bajeti iliyopita, Mkoa wa Geita ulipewa malengo ya kukusanya Sh270 bilioni na kuvuka lengo hadi kukusanya Sh328 bilioni, jambo ambalo linadhihirisha kuwa mkoa huo ni wa kimadini.
Akizungumzia ujenzi wa maabara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara (GST), Notka Banteze amesema maabara itakayokuwepo itafanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali ikiwemo madini ya dhahabu, madini ya vito na utafiti wa madini mbalimbali.
Pia, itafanya tafiti za uchenjuaji na utambuzi wa madini kwa kutumia darubini ambapo watakuwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutoa majibu kwa wateja sanjari na kuchunguza sampuli za mazingira.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dk Mussa Budeba amesema uwepo wa maabara hiyo sio tu itawaondolea usumbufu wachmbaj bali itasaidia taarifa zote za kijiolojia kupatikana Geita.