Dar es Salam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa siku 10 baadhi ya mikoa ikitarajiwa kupata mvua nyepesi, huku mingi zaidi ikitarajiwa kushuhudia hali ya ukavu.
Taarifa hiyo ya TMA kwa siku 10 kuanzia leo Alhamisi Agosti 21, 2025 hadi Agosti 31, 2025, inaonyesha mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwamo ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyuna Mara kutakuwa na hali ya ukavu.
“Nyanda za juu kaskazini-mashariki yenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro hali ya ukavu kwa ujumla inatarajiwa,” taarifa hiyo ya TMA imeeleza.
Kwa upande wa Pwani ya kaskazini, hali ni tofauti kwa sababu taarifa ya TMA inaonyesha mikoa ya Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba, kutashuhudiwa hali ya mvua nyepesi katika maeneo machache.
Nako Magharibi mwa nchi kwa mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora hali ya ukavu inatarajiwa.
“Kanda ya kati mikoa ya Dodoma na Singida hali ya ukavu inatarajiwayanda za juu Kusini-magharibi mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa hali ya ukavu inatarajiwa.
Pia, pwani ya kusini yenye mikoa ya Mtwara na Lindi kunatarajiwa hali ya ukavu kwa ujumla huku kanda ya kusini, Ruvuma na maeneo ya kusini mwa Morogoro hali kama hiyo ikitarajiwa pia,” taarifa ya TMA imeeleza.
Kutokana na hali hiyo, Mtalamu wa Mazingira, Kunda Sikazwe ameshauri wananchi wa mikoa husika kuhifadhi maji ya kutosha na malisho kwa ajili ya wanyama.
“Chakula walichonacho waitumie vizuri kama wanaweza kuhifadhi vitu kama mboga za majani wafanye hivyo, kwa upande wa kilimo wale walio karibu na mito au wenye visima na mabwawa wamwagilie mimea yao isikauke,” amesema.
Kwa upande wa afya, amesema jua litakuwa kali hivyo wanaofanya kazi shambani wazifanye asubuhi na ikifikia saa nne wafanye kazi kivulini na watumie wanywe maji mengi na vinywaji vingine.
Kwa saa 24 zijazo TMA imesema kutashuhudiwa upepo wa pwani ambao unatarajiwa kuvuma kwa kasi ya km 30 kwa saa kwa Pwani yote.
Upepo huo utavuma kutoka Kusini Mashariki kwa Pwani ya Kusini na kutoka Kusini kwa Pwani ya Kaskazini na hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa kiasi.