Hongera Simba Queens kwa kujivua gamba usajili

KATIKA dirisha linaloendelea la usajili, Simba Queens imejilipua hasa kwa kuacha majina mengi makubwa ambayo mengine hayakutegemewa kama yangeweza kupigwa chini.

Mfungaji Bora wa kikosi hicho kwa msimu uliopita, Jentrix Shikangwa ni miongoni mwa mastaa ambao wamepewa mkono wa kwaheri na Simba Queens ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara.

Nimeona pia nyota aliyedumu kwa muda mrefu katika kikosi cha timu hiyo, Asha Djafar naye amepewa Thank You na Simba Queens kama ilivyo kwa Precious Christopher, Wincate Kaari, Reticia Nabbosa, Saiki Atinuke, Mwanahamisi Gaucho, Gelwa Yona na Carolyne Rufa.

Unaweza kuishangaa Simba kwa kuwaacha baadhi ya wachezaji ambao kiuhalisia walikuwa na kiwango kizuri lakini hadi kunapotokea panga kama hilo kunakuwa na sababu za msingi.

Kwa tathmini tuliyoifanya hapa kijiweni, Simba Queens imefanya uamuzi sahihi sana wa kuachana na wachezaji hao ambao wengi wana majina makubwa katika soka la wanawake hapa nchini.

Hao wachezaji wengi wamekuwa wakicheza kwa kuridhika katika siku za hivi karibuni na ni kama wameshamaliza kila kitu, hawana njaa wala kiu ya mafanikio sasa unapokuwa nao wengi kwenye timu haiwezi kufanya vizuri.

Unapokuwa na wachezaji wa dizaini hiyo utajikuta unaingia hasara tu ya kuwalipa mishahara na stahiki nyingine huku ukiwa hupati mafanikio ama ya kutwaa taji au ya kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake ambayo yataifanya timu angalau irudishe sehemu ya gharama.

Kuacha kundi kubwa la hao wachezaji inamaanisha Simba Queens sasa inaanza upya projekti ya kutengeneza kikosi chake na kuingiza kundini wachezaji ambao wana kiu ya mafanikio na wanaohitaji kuandika historia zao.

Inawezekana projekti hiyo isizae matunda ndani ya muda mfupi lakini itaisaidia timu kwa muda mrefu muhimu wawe wavumilivu tu.