Vodacom yavuna faida ya Sh90.5 bilioni

Dar es Salaam. Kuongezeka kwa wateja na mapato ya huduma zimetajwa kuwa sababu zilizofanya kampuni ya Vodacom kurekodi faida ya zaidi ya Sh90.5 bilioni baada ya kodi.

Hayo yamebainishwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa, ambao walitajiwa kwamba rekodi hiyo imewekwa katika mwaka wa fedha wa Vodacom ulioishia Machi 31, 2025.

Hivyo, wanahisa hao wameidhinisha gawio la Sh20.20 kwa kila hisa, sawa na ongezeko la asilimia 69.3 ikilinganishwa na mwaka uliopita, kutokana na ongezeko kubwa la mapato na faida ya kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo, Alhamisi Agosti 21, 2025, mapato ya huduma za Vodacom yameongezeka kwa asilimia 20.5 na kufikia Sh1.5 trilioni, yakichochewa na ongezeko la wateja na matumizi ya huduma, hususan M-Pesa na huduma za data.

Hali hiyo imefanya faida halisi baada ya kodi kupanda kwa asilimia 69.4 hadi kufikia Sh90.5 bilioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Bisiimire, amesema faida hiyo pia imechangiwa na mikakati ya kupunguza gharama iliyookoa Sh59 bilioni, pamoja na ongezeko la wateja wapya wapatao milioni tatu na kufanya jumla wafikie milioni 22.6 mwishoni mwa mwaka huu.

Katika upande wa mapato, huduma za M-Pesa zimeongezeka kwa asilimia 29.3, huku thamani ya miamala ikipanda kwa asilimia 33.8 mwaka hadi mwaka.

Aidha, amesema matumizi ya simu janja yameongezeka kwa asilimia 33.4 na kuchochea upatikanaji wa huduma za kidijitali.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kampuni pia imejenga minara 471 ya 4G, ikiwamo 126 katika maeneo ya pembezoni kwa ushirikiano na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

“Ukuaji huu ulitokana na huduma bunifu za M-Pesa kama vile M-Koba, jukwaa la akiba kwa vikundi linalohudumia zaidi ya wateja milioni 1.3, pamoja na M-Wekeza, huduma ya uwekezaji kwa simu ambayo imekusanya amana za takribani Sh25 bilioni ndani ya miezi michache tangu kuzinduliwa,” amesema Bisiimire.

Ameongeza kuwa matokeo hayo ya kifedha na kiutendaji yanaonesha ukuaji imara, uwekezaji wa kimkakati na dhamira ya kampuni ya kuwawezesha watu, kulinda mazingira na kudumisha uaminifu.

Kwa mujibu wake, huduma ya malipo ya kidijitali ya Lipa kwa Simu imekuwa ikichakata zaidi ya Sh1 trilioni kila mwezi, huku mikopo ya muda mfupi na huduma ya Songesha ikikopesha zaidi ya Sh3 trilioni, na hivyo kusaidia wateja na wafanyabiashara nchini kote.

Aidha, amesema mapato ya huduma za data pia yameongezeka kwa asilimia 21.6, yakichangiwa na ongezeko la matumizi ya simu janja na uwekezaji katika miundombinu ya mtandao.

“Utendaji wetu mwaka huu unaonesha nguvu ya mkakati wetu na dhamira thabiti ya kuwaunganisha Watanzania na kesho iliyo bora. Kupitia ubunifu na ushirikiano, tunaziba pengo la kidijitali na kifedha,” amesema Bisiimire.

Akitaja mchango wa kampuni katika jamii, Bisiimire amesema nusu ya watumiaji wa huduma ya M-Koba ni wanawake, jambo linalodhihirisha nafasi ya Vodacom katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Amesema huduma ya M-Wekeza nayo imesaidia kupanua fursa za uwekezaji na kukuza ujumuishwaji wa kifedha nchini.

“Hivyo, tunapoadhimisha miaka 25 ya kuleta mabadiliko chanya kwa maisha ya Watanzania, tutaendelea kujikita katika ukuaji endelevu unaoongozwa na dhamira yetu,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Vodacom Tanzania, David Tarimo, amesema matokeo hayo ni ushahidi wa imani kubwa kutoka kwa wateja na wanahisa.

“Kampuni itaendelea kushirikiana na Serikali kuboresha viwango vya maisha ya wananchi kupitia huduma za mawasiliano na upatikanaji wa huduma za kifedha nchini kote,” amesema Tarimo.