Iringa. Mkulima Philimo Lalika (49) inadaiwa ameuawa kwa kuchomwa kisu tumboni na mke wake, Elizabeth Kihombo (46), katika kile kilichoelezwa kuwa ni ugomvi uliotokana na wivu wa mapenzi.
Tukio hilo limelotokea Agosti 20, 2025 katika Kijiji cha Ihefu, Kata ya Mdabulo, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 21, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi ameeleza kwamba mtuhumiwa alijaribu kujiua kwa kunywa sumu aina ya Organfosphet (dawa ya kuhifadhi nafaka) na lakini aliokolewa na sasa amelazwa katika Kituo cha Afya cha Mdabulo akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Kamanda Bukumbi amedai kuwa tukio hilo lilitokea usiku wakati wanandoa hao walipokuwa wakielekea kulala na mzozo uliibuka.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limeeleza kuwa linaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda raia na mali zao.
”Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda raia na mali zao kwa kutoa elimu na kufanya operesheni mbalimbali za kupambana na uhalifu,” imeeleza taarifa ya Kamanda Bukumbi.
Awali, akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Digital, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihefu kata ya Mdabulo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Chesco Mhwagila amesema baada ya ndugu wa familia ya Philimo Lalika na Elizabeth Kihombo kuhojiwa kuhusu wanandoa hao walidai kuwa miezi sita ya nyuma yalitokea mabishano ya kati yao lakini walifanikiwa kukaa nao chini kwa pamoja na kumaliza mgogoro huo.
“Baada ya kutokea kwa mgogoro wa wanandoa hao miezi sita ya nyuma familia ilifanikiwa kusuluhisha baada ya hapo hakukuwa na mgogoro wowote na majirani, ndugu na viongozi hatujapata taarifa ya kuwepo na mgogoro wa kifamilia kwa wanandoa hao lakini leo hii tumepata taarifa hii,” amesema Mhwagila.
“Wanandoa pamoja na familia wajitahidi kutumia vyombo vya sheria ambavyo vitawasaidia ikiwemo viongozi wa madhehebu mbalimbali kutatua migogoro kuliko kujichukulia sheria mkononi,” amesema.
Mhwagila amesema kwa miaka 15 iliyopita hilo tukio la tano kutokea katika kijiji hicho huku akisema marehemu ameacha watoto 11 na mtuhumiwa ataendelea kushikiliwa na vyombo vya sheria kuhusiana na tukio hilo.