WANANCHI ARUSHA WAPEWA ELIMU KUHUSU MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YA UMEME

…………….

Wananchi wa Mkoa wa Arusha wameelimishwa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia umeme kupitia kampeni maalum ya maonesho ya moja kwa moja yaliyofanyika katika mitaa mbalimbali ya mkoa huo. 

Kampeni hiyo inalenga kuchochea matumizi ya nishati safi kwa asilimia 80 ya kaya nchini ifikapo mwaka 2034.

Kampeni hiyo inaendeshwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na UKAid na Modern Energy Cooking Services (MECS), ikiwa na lengo la kupunguza utegemezi wa nishati chafu kama kuni, mkaa na gesi, ambazo zimekuwa zikiathiri afya na mazingira.

Katika maonesho hayo ya elimu ya vitendo, wananchi walijifunza kuhusu urahisi na faida za kutumia umeme kama nishati ya kupikia. Baadhi ya washiriki kama Daniel Edward na Ashura Derickvck wamesema wamehamasika kuachana na matumizi ya kuni na mkaa baada ya kushuhudia kwa macho teknolojia hiyo safi na nafuu.

Mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wa Arusha umeonesha mabadiliko ya mtazamo kuhusu nishati safi, huku wengi wao wakionesha nia ya kubadili mfumo wao wa kupikia majumbani.

Kampeni hiyo ya elimu itaendelea katika mikoa mingine nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhakikisha Watanzania wote wanapata elimu ya matumizi salama, rafiki kwa mazingira na endelevu ya nishati safi ya kupikia.