Fadlu ashusha mkwra mzito Misri, awataja mastaa

SIMBA mpya inapikwa huko Cairo Misri na juzi umempiga mpinzani mwingine wakati ikitesti mitambo, lakini kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids ametuma salamu kwa wapinzani, huku akishusha mkwara mzito kwa mastaa wa timu hiyo wakati wanamalizia kambi ya mazoezi wakiwa nchini humo.

Kocha huyo alisema kama kuna staa ambaye anaamini ana nafasi kikosini kutokana jina na rekodi zake za msimu uliopita, asahau kwani anaenda kuanza upya kutengeneza kikosi kazi cha kumpa matokeo mazuri katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Misri, Fadlu alisema kwamba hakuna mchezaji ambaye kwa sasa ana uhakika wa namba katika kikosi hicho na kwamba kila staa aliyepo anatakiwa kuanza upya kupigania nafasi.

“Kilichotokea au kufanyika, msimu uliopita ni historia, hapa tunaanza upya, tuna wachezaji wapya na wale ambao walikuwepo, wote wanatakiwa kujipanga upya kujitafutia nafasi.”

Simba imesajili wachezaji wapya karibu 10 akiwamo Naby Camara, Alassane Kante, Jonathan Sowah, Neo Maema, Mohammed Bejaber, Rushine de Reuck, mbali na wazawa Charles Semfuko, Morice Abraham, Anthony Mligo, Wilson Nangu na kipa Yakoub Suleiman wanaoitumikia Stars kwa sasa.

Kuhusu mechi zinazoendelea kuchezwa Misri, kocha Fadlu amesema katika mechi walizocheza hadi sasa, matokeo kwao wala sio ishu kubwa, bali kuna mambo makubwa muhimu wanayapima kwa wachezaji wao.

Fadlu alisema katika mechi walizocheza hadi sasa zimewasaidia kupima utimamu wa ufiti wa wachezaji wake na kujiridhisha kwamba wako sawasawa na kwamba kazi inayofuata kwa sasa itakuwa ni mtihani mgumu kwa wapinzani watakaokutana nao katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.

Juzi, Simba iliipiga Al Zulfi ya Saudi Arabia kwa bao 1-0, likifungwa na kiungo na mfungaji bora wa timu hiyo msimu uliopita Jean Charles Ahoua kwa mpira wa friikiki, ikiwa ni mechi ya tatu kwao baada ya awali kushinda 2-0 mbele ya Kahraba Ismailia na kupoteza 4-3 mbele ya ENPPI.

“Hatuangalii sana matokeo, lakini yapo mambo tunayapima kama yako sawasawa kwenye hizi mechi, nafurahi kuona utimamu wa mwili kwa wachezaji uko sawasawa, hili ni muhimu kwa hatua ya kwanza,” alisema Fadlu na kuongeza;

“Tutakuwa na mechi za karibu karibu katika Ligi, tumekuwa tunacheza hizi mechi kwa karibu kuangalia kama wachezaji wanaweza kuhimili na kila kitu kipo sawasawa.

Kocha huyo alifichua kuwa jana wachezaji walikuwa katika mapumziko ya siku moja kabla ya leo kurejea tena kwa lengo la kujenga mbinu za uwanjani ikiwa ni hatua ya kuelekea mwisho wa kambi yao.

Alisema katika eneo hilo watapambana kutengeneza kemia kwa wachezaji wao katika idara zote.

“Tunakwenda sasa kuanza kutengeneza mbinu uwanjani, hii ni ratiba ambayo itafuata baada ya mapumziko ya leo (jana), hapa tutakuwa na ubora wa kuamua tunachezaje dhidi ya nani,” alisema Fadlu na kuongeza;.

“Tutatumia muda mrefu hapa kwa kuwa ndio eneo la mwisho lakini umeona tumekuwa tunawasili kwa makundi tofauti na wengine bado hawako hapa, tutaimarisha pia muunganiko wa timu kiujumla.”