KAMA ulikuwa hufahamu kuna miezi kadhaa Yanga ilikuwa inajifua ikitumia viwanja vya kukodi, lakini juzi kikosi hicho kilirudi rasmi kambi yao iliyozoelekea lakini iliyokarabatiwa upya pale Avic Town, Kigamboni, jijini Dar es Salaam baada ya kocha wa timu hiyo, Romain Folz kufanya maamuzi.
Kama hujui ni kwamba Yanga huwa ikitokea hapo hakuna timu ya ndani iliyoisumbua ikiwemo Simba ambayo inatarajiwa kukutana nayo Septemba 16 katika mechi ya Ngao ya Jamii kuzindua msimu wa 2025-26.
Kocha wa Yanga amefuta hesabu za kuweka kambi nje na kama haitoshi, ameridhika na mandhari ya Avic ambako tangu ianze kutumia kambi hiyo imepoteza mara mbili tu dhidi ya Simba, lakini yenyewe ikishinda mara tano mfululizo.
Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga, ilikuwa Agosti 16, 2023 katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Mkwakwani, Tanga kwa ushindi wa penalti 3-1 baada ya mechi hiyo kumalizika kwa suluhu, mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa kocha Miguel Gamondi.
Nyuma yake Yanga ikipoteza kwa mabao 2-0, ukiwa ni mchezo wa ligi Aprili 16, 2023 wakati huo kocha wao alikuwa Nasredine Nabi na Wekundu hao walikuwa na Mbrazil Roberto Oliveira ‘Robertinho’, mechi zote hizo mbili zilifuatana flani.
Baada ya hapo Yanga ikitokea hapo Avic imeshinda mara tano mfululizo, huku kuna mara tatu ilitoa sare, ikiwa ni kambi yao ya jeuri.
Yanga ilikuwa na hesabu tofauti za kwenda kuweka kambi nje, ambapo hesabu za mwisho ilikuwa kwenda Misri kule Alexandria Jiji flani la kitalii.
Baada ya Simba kwenda Misri, safari hiyo ni kama ikaingia ‘mdudu’ kwa mabosi wa Yanga kuona kama hatakuwa sawa nao kwenda, huko licha ya kwamba Wekundu hao wapo jiji tofauti la Cairo baada ya awali kuanzia Ismailia lililopo umbali wa kilometa 337 kutoka Alexandria.
Taarifa rasmi ni kwamba sasa Yanga imejichimbia Avic kuanzia juzi na itatokea hapo kuifuata Simba katika pambano la uzinduzi wa msimu mpya wa mashindano nchini kwa mwaka 2025-26 la Ngao ya Jamii litakalopigwa Septemba 16 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Awali, mabosi wa Yanga walimuonyesha kocha wao Romain Folz ubora wa Avic, lakini kama haitoshi wakampa rekodi yao kwamba eneo hilo tangu waanze kulitumia hakuna timu ya ndani imewasumbua na Mfaransa huyo akakubaliana nao na kuamua kuizuia timu hiyo isisafiri tena kwenda nje ya nchi.
“Tumefuta hiyo safari, kwenye kambi yetu kuna ukarabati mkubwa umefanyika, ilikuwa hata kama tungetoka nje ya nchi tungetudi pale, lakini kwa mabadiliko yaliyofanyika, tumekubaliana tutamalizia maandalizi yetu hapo na uzuri kocha ameridhia,” alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga.
“Hatuangalii tu rekodi sisi hakuna timu imetusumbua tukitokea Avic, hata hao Simba wanajua na tutawathibitishia tena hili Septemba 16 na kocha amekubali kwamba panatosha.”