Taifa Stars twen’zetu nusu fainali CHAN 2024

LEO Ijumaa, timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ina mchezo muhimu katika michuano ya CHAN 2024 itakapoikaribisha Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku mazingira ya timu hiyo kufanya vizuri yakiwekwa sawa.

Mchezo huo uliopangwa kuanza saa 2:00 usiku, Taifa Stars ni mara ya kwanza inacheza hatua ya robo fainali, wakati wapinzani wao wakionekana kuwa wazoefu kwani tayari wamebeba ubingwa mara mbili, 2018 na 2020.

Licha ya Morocco kuonekana kuwa tishio katika mchezo huo, lakini Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman amebainisha hakuna cha kuhofia na kwenye uwanja wa mazoezi wameyafanyia kazi mapungufu yaliyokuwepo ikiwemo kutumia nafasi za kufunga.

“Tunawaheshimu, lakini hatuogopi, najua Uwanja wa Benjamin Mkapa utajaa kwa sababu Watanzania sasa wanaiamini timu yao,” alisema kocha huyo na kuongeza.

“Suala la kutumia nafasi tunaendelea kuhakikisha tunapambana nalo kwani kabla ya mashindano nilisema tuna tatizo eneo hilo, lakini kila kitu kinahitaji muda kukaa sawa.

“Ukiangalia tumefunga mabao matano hatua ya makundi, sasa tupo robo fainali na ni mechi za maamuzi, hivyo lazima tufunge, ndiyo maana mazoezini tunafanya sana mazoezi ya kutumia nafasi, jambo zuri ni wachezaji wanafanya mazoezi vizuri kwa kufuata maelekezo, naamini mchezo huu tutafunga mabao.”

Taifa Stars imeongoza Kundi B kwa kukusanya pointi 10 baada ya kushinda mechi tatu na sare moja ikifunga mabao matano na kuruhusu moja, wakati Morocco ilishika nafasi ya pili Kundi A na pointi tisa, ikishinda mechi tatu na kupoteza moja. Imefunga mabao manane na kuruhusu matatu.

STA 04


Takwimu zinaonyesha ukiweka kando uimara wa kila timu katika maeneo ya ndani ya uwanja ambapo Taifa Stars inalinda vizuri lango lake ikiruhusu bao moja pekee, wakati Morocco ina safu kali ya ushambuliaji ikifunga mabao manane, lakini zote zinaonekana kutumia vizuri kipindi cha pili.

Katika mabao matano iliyofunga Tanzania, matatu yamepatikana kipindi cha pili huku mawili cha kwanza. Morocco nayo kipindi cha pili imefunga matano, huku kile cha kwanza yakiwa matatu.

Stars hadi sasa katika kucheka na nyavu imebebwa na Clement Mzize aliyefunga mabao mawili, huku Abdul Suleiman Sopu, Mohamed Hussein na Shomari Kapombe kila mmoja akifunga moja.

Oussama Lamlioui ndiye silaha muhimu kwa Morocco kutokana na kufunga mabao matatu, huku Mohamed Rabie Hrimat akipachika mawili. Imad Riahi na Sabir Bougrine wakifunga moja kila mmoja. Pia wana bao moja lililotokana na Quinito wa Angola kujifunga.

STA 01


Kitendo Taifa Stars kutinga robo fainali ya michuano ya CHAN 2024 kiliihakikishia timu hiyo Dola 450,000 ambazo ni zaidi ya sh1.1 bilioni, hata hivyo, vijana hao wa Hemed Suleiman ‘Morocco’ wanakabiliwa na kibarua kingine leo Ijumaa kinachoweza kuwahakikishia mkwanja mrefu zaidi.

Michuano ya CHAN PAMOJA 2024 imepata ongezeko kubwa la zawadi hivyo mabingwa wa michuano hii watavuna Dola 3.5 milioni (zaidi ya Sh9.1 bilioni), ongezeko la asilimia 75 ukilinganisha na zile za awali. Huku jumla ya bajeti ikiongezeka hadi Dola 10.4 milioni.

Kama Stars itaitupa nje Morocco ambao ni mabingwa mara mbili wa mashindano hayo, itakuwa imepata ongezeko la Dola 150,000 ambazo ni zaidi ya Sh375milioni hivyo jumla itakuwa na zaidi ya Sh1.5 bilioni.

Mkwanja huo ni kwa timu itakayomaliza nafasi ya nne kwenye mashindano hayo, lakini kama itashika nafasi ya tatu basi itakuwa na uhakika na Dola 700,000 zaidi ya Sh1.75 bilioni, ikishika nafasi ya pili ni Dola 1.2 milioni ambazo ni zaidi ya Sh3 bilioni.

Msimu uliopita wa mashindano ya CHAN 2022 ambayo yalifanyika Algeria, Senegal ilitwaa ubingwa na kujikusanyia Dola 2 milioni ambazo ni zaidi ya Sh5 bilioni.

STA 02


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewazawadia Taifa Stars Sh200 milioni kwa ajili ya mchezo wa robo fainali dhidi ya Morocco.

Fedha hizo zimewasilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, alipoitembelea timu hiyo kambini jijini Dar es Salaam, jana Agosti 20, 2025, na kuwapongeza kwa hatua kubwa waliyofikia pamoja na kuwatakia heri kwa mchezo ujao.

STA 03


Kabla ya kushuhudia Taifa Stars ikikabiliana na Morocco, itatanguliwa na mechi kati ya Kenya dhidi ya Madagascar itakayochezwa kwenye Uwanja wa Moi International Sports Centre uliopo Nairobi, Kenya kuanzia saa 11:00 jioni.

Kenya kama ilivyo kwa Tanzania, nayo imeongoza Kundi A ikikusanya pointi 10, wakati Madagascar ilikuwa ya pili Kundi B na pointi zake saba.

Mchezo huu ni wa tofauti kidogo, Kenya imekuwa wazuri kufunga mabao kipindi cha kwanza na imepachika matatu na cha pili ikifunga moja. Wafungaji wao wakiwa ni Austin Odhiambo na Ryan Ogam ambao kila mmoja amefunga mawili.

Madagascar yenyewe imefunga zaidi kipindi cha pili. Katika mabao matano, kipindi cha kwanza imefunga mawili na cha pili matatu.

Lalaina Rafanomezantsoa ndiye kinara wao akifunga mawili, huku Mika Razafimahatana, Toky Niaina Rakotondraib na Fenohasina Gilles Razafimaro wakifunga mojamoja