TIMU ya Singida Black Stars inaendelea na maandalizi ya msimu jijini Arusha chini ya kocha Miguel Gamondi, huku uongozi wa kikosi hicho ukifikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji, Andrew Phiri kutoka Maestro United ya Zambia.
Nyota huyo raia wa Zambia, alikuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichotolewa katika michuano ya CHAN 2024, ambapo mabosi wa Singida wamefikia makubaliano hayo, huku ikielezwa amesaini mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mmoja.
Mtu wa karibu na mchezaji huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, aliliambia Mwanaspoti Phiri alimpa taarifa za kujiunga na Pamba Jiji, ingawa dili hilo lilikwama mwishoni baada ya mabosi hao wa kikosi hicho cha TP Lindanda, kuachana naye.
“Viongozi wa Pamba walipokuja Zambia kufanya mazungumzo na Larry Bwalya waliwasiliana naye na kuonyesha nia ya kumtaka pia, japo walionekana hawako siriasi na mchezaji kuamua kutafuta changamoto sehemu nyingine,” kilisema chanzo hicho.
Phiri aliyezaliwa Mei 21, 2001, tofauti na Pamba Jiji iliyomuhitaji, timu nyingine za Yanga, Simba na Azam FC ni kati ya zilizoonyesha nia ya kumuhitaji katika vipindi mbalimbali, ingawa ni Singida ambayo imeinasa saini yake.
Nyota huyo alihudhuria majaribio katika timu ya Orlando Pirates ya Afrika ya Kusini Machi 2025, huku akimaliza mfungaji bora wa Maestro United kwa kipindi cha misimu minne mfululizo, na ameifungia pia mabao 69, kwenye mashindano yote.
Mwanzoni mwa msimu, nyota huyo alikuwa anahusishwa na timu za Zesco United na Power Dynamos zote za kwao Zambia, baada ya kuonyesha kiwango kizuri kilichoivutia miamba hiyo, huku msimu wa 2023-24, alichaguliwa mchezaji bora wa msimu.