KOCHA wa timu ya taifa la Sudan, Kwesi Appiah amesema wako tayari kwa robo fainali ya CHAN 2024 watakapokutana na Algeria ambao ni wanafainali za mwaka 2022.
Sudan ilimaliza nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa kundi D ikiwa na pointi tano sawa na Senegal huku Algeria ikishika nafasi ya pili kundi C na pointi sita moja nyuma ya Uganda.
“Kutinga hatua za juu kunamaanisha kuna michezo migumu zaidi. Mechi ya Senegal imeshapita, tunaufikiria ujao dhidi ya Algeria. Haitakuwa rahisi, lakini tutapambana,” alisema.
Licha ya Sudan kufanya maandalizi siku nne tu kabla ya mashindano hayo kuanza, ni moja ya timu zilizoshangaza wengi baada ya kuichapa Nigeria mabao 4-0, hatua ya makundi na sare dhidi ya bingwa mtetezi, Senegal.
Akiongelea sapoti waliyoipata Zanzibar walikocheza mechi zao za makundi na watacheza robo hapo kesho, Jumamosi dhidi ya Algeria kocha huyo alisema;
“Watu wa Zanzibar wanafanana na Wasudani. Wanaongea Kiarabu, hivyo kulikuwa na uhusiano mzuri tulipoingia.”
Katika mechi tano zilizopita kati ya timu hizi mbili za mashindano yote ikiwemo mechi za kirafiki, Algeria imekuwa na matokeo chanya zaidi dhidi ya Sudan, ikifunga jumla ya mabao 7-0 katika michezo miwili ya hivi karibuni ya mwaka 2021 na 2022.
Hata hivyo, Sudan inarekodi nzuri katika CHAN dhidi ya timu hiyo kwani Februari 2011 ilishinda bao 1-0.