Watoto watatu wafariki dunia kwa jiko la mkaa

Busega. Watoto watatu wa kike wamefariki dunia baada ya kukosa hewa safi wakiwa ndani ya hema walilokuwa wamelala, baada ya kuwasha jiko la mkaa kwa ajili ya kupika uji wakati wa kambi ya waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato katika Kijiji cha Mkula, Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu.

Tukio hilo limetokea Agosti 18, 2025 na kuhusisha watoto Loveness Kilonzo (9), Mary Jackson (12) na Pasheni Yusuph (14) ambao ni wanafunzi  katika Shule ya Msingi Masangani iliyopo wilayani humo.

Kutokana na ajali hiyo ya moto Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (RC), Anamringi Macha ameagiza kusitishwa kambi hiyo na kuwataka viongozi wa dini mkoani humo kutoa taarifa mapema kwa Serikali ya mkoa ili kushirikiana kuimarisha usalama wa watoto wanapohitaji kuweka makambi ya kidini.

Mkuu wa Mkoa wa Macha amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa chanzo cha vifo hivyo ni moshi wa mkaa lililokuwa ndani ya hema.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na uongozi wa kanisa wamesitisha kambi hiyo na wataweka utaratibu mpya wa usalama kabla ya kuruhusu makambi mengine kuendelea.