Russia. Zipo baadhi ya dawa za matibabu ambazo zina faida kubwa katika kukabiliana na matatizo ya kiafya lakini huwa na madhara machache yenye hatari ndogo ikiwamo hali ya kulewa, kulevya au hali ya usingizi.
Kitabibu madhara haya machache si lazima yamtokee kila mtu; hii ni kwasababu kila mtu huwa na ustahimilivu wa kibaiolojia wa upokeaji dawa mwilini.
Ni kawaida pia mwili kukutana na changamoto ya kushindwa kuhimili madhara machache yatokanayo na dawa hizo.
Dawa ambazo zinaweza kusababisha kusinzia au hali yakulevya ni pamoja na dawa za kukabiliana na magonjwa ya akili, mzio, kikohozi na mafua, maumivu na za magonjwa ya moyo.
Endapo mtumiaji wa dawa hizi atakuwa na majukumu kama vile kuendesha vyombo vya moto pamoja na kudhibiti mitambo, itamlazimu kuacha kuendesha mpaka atakapomaliza dozi yake.
Mfano dawa za kuzuia mzio jamii ya Antihistamines, maarufu kama piriton hutumika mara kwa mara kukabiliana na mzio. Huwa na hali ya kulewa usingizi.
Dawa za magonjwa ya akili ikiwamo za kudhibiti mfadhaiko, zinaweza kusababisha kusinzia au hali ya kulewa na uchovu.
Mfano wa dawa jamii ya valiamu, hizi hutumika kwa ajili ya maumivu, kutuliza wasiwasi na kifafa au degedege hujulikana zaidi kwa athari ya kusababisha kusinzia.
Antipsychotics, dawa hizi za kukabiliana na matatizo ya akili, pia zinaweza kusababisha kusinzia.
Dawa kali za maumivu zenye opiod kama vile Tramadol ambazo zinaweza kusababisha kusinzia sana au hali ya kulewa.
Vile vile dawa kutuliza misuli ikiwamo vipumzisha misuli vingi vinaleta athari za usingizi lakini huwa ni athari ndogo ya kuvumilika.
Zipo pia dawa nyingine, ikiwamo dawa kama za shinikizo la damu kama vile beta-blockers na baadhi ya dawa za ugonjwa wa Parkinson yaani kutetemeka pasipo hiari zinazoweza kusababisha kusinzia.
Dawa hizi zinaweza kutoa athari sawa na pombe kutokana na athari zake kwenye vipokezi vya GABA kwenye ubongo na kipitishio cha neva za fahamu kinachohusika katika kudhibiti utulivu na utulizaji.
Dawa nyingine ikiwamo baadhi ya dawa za kutuliza mafua na kikohozi zenye hali ya maji maji huweza kuleta hali ya kulevya au kusinzia.
Ni muhimu kuelewa kwamba ingawa dawa hizi zinaweza kuwa na athari za pombe, zinaweza pia kuja na madhara yao wenyewe, ikiwamo kizunguzungu, udhaifu na maumivu ya tumbo.
Kama Ilivyo pombe, baadhi ya dawa hizi zinaweza pia kusababisha utegemezi na uraibu.
Habari nzuri ni kuwa dawa hizi zina faida kubwa katika matibabu kuliko madhara machache yanayojitokeza. Inashauriwa kuepuka kutumia dawa za makundi haya kiholela pasipo ushauri wa daktari.
Hakikisha unazingatia maelekezo ya daktari au yale yaliyomo katika kijikaratasi ndani ya boksi la dawa.