Kiwanda cha uchakataji zao la kakao chanukia Kyela, wakulima kicheko

Mbeya. Chama Kikuu cha Ushirika Kyela (Kyecu), kimesema wakati kikiendelea kutafuta soko ndani na nje ya nchi kwa mazao ya kimkakati wilayani humo, kinatarajia kujenga kiwanda kwa ajili ya kuchakata na kuongeza thamani kwa zao la kokoa ili kuleta bei shindani kwa kilimo hicho.

Hii ni baada ya zao hilo na mengine wilayani humo kuonekana bei yake kutokuwa nzuri katika soko la kimataifa kufuatia uzalishaji mkubwa kwa nchi za Afrika ya Magharibi na kukosa watumiaji wa ndani, hivyo uwapo wa kiwanda hicho unatarajia kupanua wigo kwenye soko na thamani kwa kilimo hicho.

Wilaya ya Kyela ni maarufu kwa kilimo cha Kakao, ambacho kimekuwa sehemu ya uchumi kwa wananchi wilayani humo, huku mazao mengine ya kimkakati ikiwa ni ufuta na mbaazi.

Katika minada ya hivi karibuni, Kyecu iliuza tani 55 kwa zao la Mbaazi ambapo kilo moja ilikuwa Sh 810, huku ufuta ikiuza kwa Sh2,450 kwa bei ya juu na kokoa ikiuzwa kwa Sh18,600 kwa kilo moja.

Akizungumza leo Ijumaa Agosti 22, kaimu meneja wa chama hicho, Nabii Mwakyenda amesema kutokana na kushuka kwa bei ya mazao hayo mwaka huu, wanatarajia kujenga kiwanda kwa ajili ya kuchakata zao la kakao ili kuleta bei shindani.

Amesema Kyecu imekuwa ikitegemea zaidi soko la nje kutokana na kukosa watumiaji wa ndani, akieleza kuwa nchi za Magharibi zimekuwa zikiathiri zaidi zao la kokoa kwa Tanzania.

“Kutokana na uzalishaji mkubwa wa zao la Kokoa kwa nchi za Afrika Magharibi, imesababisha changamoto kwetu tunaozalisha kwa kiwango kidogo, hivyo Kyecu inaangalia uwezekano wa kuwa na kiwanda chetu.

“Tukiwa na kiwanda chetu tutaweza kuchakata na kuza ghafi na kuongeza wigo kiushindani na kuwa na uhakika wa soko ndani na nje na mpango huu unatarajia kukamilika kwa kipindi cha miaka mitatu,” amesema Mwakyenda.

Meneja huyo ameongeza kuwa wakati chama hicho kikiendelea na mikakati hiyo, wakulima wilayani humo, wanapaswa kuzalisha mazao yenye ubora ili kulinda thamani na soko.

Kwa upande wake Ofisa Mipango wa Kyecu, Lwimiko Mwaijande amesema kwa mipango ya muda mfupi ni kuhakikisha mazao yote yanauzwa kwa mfumo wa stakabadhi wa mazao ghalani (TMX) na kupata ushindani sokoni.

“Kwa mipango ya muda mrefu ni kuongeza thamani ya mazao yetu tukianza na kakao, lakini mbaazi na ufuta yatafuta, japokuwa tunahitaji kuingiza mazo mengine kwenye TMX ikiwa ni mawese na mchele,” amesema Mwaijande.

Mkulima Gwakisa Mwantipa amesema bado changamoto ni kutokuwa na bei rasmi, akieleza kuwa uwapo wa kiwanda cha ndani, inaweza kusaidia kuongeza thamani na bei shindani kwa mazao kwa wakulima wilayani humo.

“Tunao uzalishaji mzuri, lakini bei ndio changamoto, hatuna kiwango maalumu, Kyecu wametusaidia na iwapo tutapata kiwanda inaweza kuondoa mkanganyiko na wakulima tukajihakikishia thamani ya mazao yetu kwa bei shindani,” amesema Mwantipa.

Naye Tulia Mwakagenda amesema bado bei ya zao la mbaazi hairidhishi ukilinganisha na mazao mengine, akieleza kuwa licha ya uzalishaji wanaomba Kyecu kuwasaidia wakulima.

“Bei ya mbaazi bei iko chini sana na haieleweki ikilinganishwa na mazao mengine, ushindani ni mkubwa kwakuwa tunazalisha kwa ubora, tunashukuru Kyecu kwa jitihada inazofanya kwa faida ya wakulima,” amesema Tulia.