Jimmyson Mwanuke kurejea Mtibwa Sugar

MTIBWA Sugar iliyopanda Ligi Kuu msimu huu imeanza mazungumzo na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Singida Black Stars, Jimmyson Mwanuke.

Kama nyota huyo atakamilisha dili hilo itakuwa mara ya pili kuichezea Mtibwa msimu wa 2023/24 kwa mkopo akitokea Simba ambako hakupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

Chanzo kililiambia Mwanaspoti kuwa viongozi wa timu hiyo wanaamini kuwa na Mwanuke ambaye amekuwa na uzoefu akiwa na Simba itawasaidia Ligi Kuu.

“Ni baadhi ya vitu vichache tu ambavyo havijakamilika lakini kuna uwezekano mkubwa wa Mwanuke kuichezea Mtibwa msimu ujao, makubaliano ya kila pande yamefikiwa,” kilisema chanzo hiko na kuongeza;

“Waliishi vizuri wakati ule kabla ya Mtibwa Sugar kushuka lakini pia inaonekana ofa waliyoweka imemshawishi mchezaji na kuna asilimia kubwa ya kucheza huko.”

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu uliopita imerejea Ligi Kuu msimu huu ikiwa bingwa wa Ligi ya Championship baada ya kumaliza kinara kwa pointi 71 katika msimamo.

Akiwa Singida msimu uliopita Mwanuke hakupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza akikumbana na ushindani wa namba kutoka kwa Arthur Bada aliyetimkia JS Kabylie.