Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imepanga Septemba 23, 2025 kutoa hukumu katika kesi ya mauaji ya mwanafamilia inayowakabili Sophia Mwenda (64) na mwanaye wa kiume Alohonce Magombola (39).
Kesi hiyo ilipangwa kutolewa hukumu hiyo leo, Agosti 22, 2025, lakini imesogezwa mbele hadi tarehe hiyo kwa kile kilichoelezwa Mahakama hapo kuwa bado hukumu hiyo haijakamilika kuandikwa.
Sophia na mwanaye wanadaiwa kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni binti yake wa kwanza wa kumzaa mwenyewe kwa kumchoma kisu chini ya titi, tukio wanalodaiwa kulitenda Desemba Mosi, 2020 eneo la Kijichi, Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam.
Leo, Wakili wa Serikali, Eric Davies amedai mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.
Davies baada ya kutoa taarifa hiyo, hakimu Makube amesema hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Mary Mrio ambaye ameongezewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi hiyo ya mauaji, bado hajamaliza kuandika hukumu.
Kutokana na sababu hiyo, Hakimu Makube aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 23, 2025 kwa ajili ya kutolewa hukumu.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la mauaji linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Julai 11, 2025 Mahakama hiyo iliwakuta na kesi ya kujibu washtakiwa hao, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.
Upande wa mashtaka uliita mashahidi 22 na vielelezo tisa ambao walitoa ushahidi wao mahakamani hapo kuhusiana na kesi hiyo ya mauaji.
Hata hivyo, mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Hilda Mushi na Godwin Fissoo, waliieleza mahakama hiyo wanatarajia kuwa na mashahidi wanne kila mmoja wakiwemo washtakiwa hao pamoja na vielelezo.
Katika utetezi wake, mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Alphonce alidai kuwa hahusiki na kifo cha dada yake.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa utetezi Hilda Mushi, Alphonce alidai kuwa hajawahi kupelekwa Bagamoyo kwenda kuonyesha askari Polisi sehemu ambayo mwili wa Beatrice ulitupwa na kama ingekuwa ni kweli basi hata mwenyekiti wa eneo hilo au askari polisi wa Bagamoyo wangekuja kutoa ushahidi wao.
Pia, amesema hajawahi kupelekwa Kijichi kwenda kuchora ramani ya tukio la mauaji kama mashahidi wa upande wa mashtaka walivyodai.
Katika ushahidi aliyotoa Sophia alidai kuwa yeye ni mfanyabiashara wa mazao na makazi yake ya kudumu ni Moshi mkoani Kilimanjaro na Mbeya.
Pia, amedai kuwa hausiki na kifo cha mwanaye kwa sababu taarifa za kifo hicho yeye alikuwa Moshi.
Lakini, pia alikamatwa Machi 17, 2022 wakati akiwa hospitali ya Zakhiem akiwa katika foleni ya kumuona daktari, hivyo hausiki na kifo cha Beatrice.
“Niliajiriwa serikalini huko mkoani Morogoro na mume wangu aliajiriwa serikali za mitaa na mwaka 1986 tulifunga ndoa na kubahatika kupata watoto wanne” alidai Sophia.
“Mwaka 1994, mume wangu alioa mke mwingine huko Mbeya na mimi sikufurahia jambo hilo, hivyo nilienda kwa Askofu kulalamika,” alidai.
Aliendelea kujitetea kuwa mwaka 1995 alinunua kiwanja mkoani Mbeya na mwaka 1996 alianza ujenzi na mwaka 1998 na baada ya hapo alienda nchini Uganda kusoma.
Shahidi huyo alidai pia alipigwa na kuteswa wakati akiandika maelezo ya onyo polisi na kupelekea kuumia jicho lake.