BEKI mpya wa Tanzania Prisons, Heritier Lulihoshi, raia wa DR Congo amesema ni jambo la furaha kwake kuendelea kukiwasha katika Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akiwashusha presha maafande hao kwa kusema anaamini mambo yatakuwa mazuri msimu mpya kuliko uliopita.
Lulihoshi amesaini mwaka mmoja ndani ya maafande hao baada ya kuachana na Dodoma Jiji aliyojiunga nayo msimu uliopita akitokea Tabora United.
Beki huyo alisema kujiunga na maafande hao ni thamani kubwa kwake kwani imempa nafasi adimu ya kuendelea kucheza kwenye ligi yenye ubora na ushindani mkubwa barani Afrika.
Alisema amejipanga kuhakikisha analipa imani aliyopewa na wajela jela hao kwa kuisaidia kufanya vizuri na kujiepusha mapema na hekaheka za kushuka dirisha zilizowakumba msimu uliopita.
“Nipo Prisons msimu huu nimesaini hapa mwaka mmoja, namshukuru Mungu nimepata nafasi ya kuendelea kufanya kazi tena Tanzania kwenye Ligi Kuu,” amesema Lulihoshi na kuongeza;
“Thamani ambayo nimeoneshwa kwa wajelajela ndio imenivutia kuungana nao na naamini utakuwa wakati mzuri kwangu na kwa timu ambayo tumeona inajaribu kuboresha kikosi na benchi la ufundi baada ya kile walichokipitia msimu uliopita.”
Beki huyo anaungana na nyota wapya waliosajiliwa dirisha hili klabuni hapo akiwemo Emmanuel Mtumbuka kutoka Mashujaa, Marco Mhilu na Neva Kaboma kutoka JKU, huku ikiwaacha Beno Ngassa na Vedastus Mwihambi.