Dar es Salaam. Wakati kukiwa na kilio cha makusanyo madogo ya kodi ikilinganishwa na shughuli za kiuchumi zilizopo, Taasisi ya sekta binafsi nchini (TPSF) imeeleza hatua ambazo zikichukuliwa zitabadilisha hali hiyo.
Akizungumza leo Agosti 22,2025 wakati wa kikao kazi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na maofisa watendaji wakuu wa kampuni zilizo chini ya TPSF, Mkurugenzi wa TPSF Raphael Maganga amepongeza hatua ya kuongeza wigo wa walipa kodi akieleza kuwa itapunguza mzigo uliopo ambao unabebwa na walipa kodi wachache wengi wakiwa wafanyabiashara.
“Kampuni kubwa Tanzania ziko 871 na ndizo zinachangia asilimia 40 ya kodi yote inayokusanywa nchini, tunaona kuna mzigo mkubwa kwa kampuni chache wakati zipo kampuni nyingi hazijachangia ipasavyo katika ulipaji wa kodi.
“Tunatambua kwamba msingi wa maendeleo ya nchi yetu ni kodi hivyo kupanua wigo wa walipa kodi ni jambo la muhimu. TRA mwaka huu ina lengo la kukusanya Sh36 trilioni kiasi hiki ni kikubwa hivyo tunahitaji mno kuongeza wigo wa wachangiaji kodi,” amesema Maganga.
Mkurugenzi huyo ameshauri kuangaliwa vyema kwa sekta za kilimo na teknolojia ili zichangie kwenye makusanyo ya kodi vile inavyostahili.
“Sekta ya kilimo inachangia asilimia 25 ya pato la Taifa, imeajiri asilimia 65 ya watanzania lakini kwenye ulipaji kodi inachangia chini ya asilimia 1 tunaona ni eneo ambalo likiwekewa nguvu linaweza kuongeza kodi. Pia kwenye teknolojia tunaona biashara nyingi kwa sasa zimeenda mtandaoni ni vyema tukaangalia ni jinsi gani hizo biashara zinaweza kuchangia kwenye kodi,”.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) Joseph Priscus ameshauri TRA kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi na wafanyabiashara ili wahamasike kulipa kodi kwa hiari.
“Hiyo elimu ishuke hadi chini, isiwe TRA ikienda vijijini wenye maduka wafunge biashara zao, inatakiwa waelimishwe ili wao wenyewe watambue umuhimu wa kulipa kodi na wajione wanawajibika kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Joseph.
Katika mkutano huo TRA imeweka wazi mkakati wake wa kukabiliana na wafanyabiashara wanaokwepa kodi ikisema hautaangalia uraia wa mtu bali kila atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Hatua hiyo ya TRA inalenga kuhakikisha Tanzania inafikia uwiano wa asilimia 15 ya mchango wa kodi kwenye pato la Taifa kama ilivyokubaliwa katika nchi za kusini mwa Afrika.
Takwimu zinaonesha kwa Tanzania kiwango hicho ni asilimia 13.7 hivyo kuwepo kwa asilimia 1.3 ya kodi ambayo hailipwi.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema ili Tanzania iweze kufikia kiwango hicho ni lazima ipambane na ukwepaji wa kodi ni hilo halitaangalia uraia wa mtu.
“Wakwepa kodi wapo wengi na tutaanza na wale wakubwa. Ieleweke tunapochukua hatua kwa mfanyabiashara mwenye asili ya nchi fulani hatupambani na hiyo nchi tunapambana na mkwepakodi na mtu anayevunja sheria za nchi.
“Ukwepaji kodi bado ni mkubwa na hapa kwetu inaonekana ni kwa asilimia 1.3, unaweza kujiuliza wanakwepaje jibu ni kwamba hawatoi risiti, wanapunguza mauzo na tuna ushahidi kuwepo kwa viwanda vinavyokwepa kodi ikiwemo vinavyozalisha vinywaji changamfu,” amesema Mwenda.
Katika hatua nyingine mamlaka hiyo imeanzisha dawati la kuwalea wafanyabiashara wadogo kuanzia wilayani hadi ngazi ya mkoa lengo likiwa ni kuwakuza ili wafikie uwezo wa kulipa kodi.
Mwenda amesema hatua hiyo inalenga kuongeza wigo wa walipa kodi ikiwa ni moja ya kilio kinachotolewa na wafanyabiashara wakieleza kubebeshwa mzigo mkubwa wa kodi ilhali kuna kundi kubwa la watu ambao hawalipi kodi.
Kamishna Mwenda amesema kwa sasa wafanyabiashara hao hawatatozwa kodi bali watajengewa misingi ya kukuza biashara zao hadi pale itakapoonekana kuna haja ya wao kuingizwa kwenye mfumo wa ulipaji kodi.
“Kila ambaye anataka kufanya shughuli za kiuchumi aje kwetu tutamsikiliza na kumuelekeza njia mbalimbali za kufanya biashara na tutahakikisha inakuwa. Hatutaanza kwa kutoza kodi naomba hilo lieleweke.
“Tunachotaka kwa sasa ni kuzirasimisha biashara, zile ambazo sio rasmi tutaziwezesha. Dawati hili litakuwa na kazi wa kuwatambua wafanyabiashara wote walio nchini hata wale wadogo kabisa ambao hawatambuliki, kuwaweka kwenye makundi na kuwalea ili wakue,”.