WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE AZINDUA MIONGOZO NA MIFUMO YA KIELEKTRONIKI YA OFISI YA WAZIRI MKUU

Na; Mwandishi Wetu – DODOMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amezindua miongozo mitatu na mifumo ya kielektroniki miwili ambayo inalenga kuimarisha uratibu, usimamizi na uendeshaji wa masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.

Miongozo na Mifumo iliyozinduliwa ni pamoja na Mwongozo wa Majadiliano baina ya Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Waajiri wa Mwaka 2025, Mwongozo wa Uratibu wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu wa Mwaka 2025, Mwongozo wa Wakala Binafsi wa Ajira wa Mwaka 2025, Mfumo wa Kitaifa wa Kieletroniki wa Taarifa za Soko la Ajira wa Mwaka 2025 na Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri ya Usuluhishi na Uamuzi wa Mwaka 2025.

Akizindua leo 22 Agosti, 2025 jijini Dodoma, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kuwa miongozo na mifumo itasaidia kujenga misingi ya majadiliano yenye tija na jumuishi, uimarishwaji wa haki za Watu wenye Ulemavu, usimamizi makini wa mawakala wa ajira, pamoja na uwepo wa mifumo ya kisasa ya kukusanya na kuchakata taarifa za soko la ajira, sambamba na kuendesha mashauri ya kazi na usuluhishi kwa ufanisi mkubwa kupitia mifumo hiyo ya kielektroniki.

Waziri Ridhiwan aliongeza kusema miongozo na mifumo iliyozinduliwa ina manufaa ya kutokomeza umaskini na kuimarisha uwezo wa wananchi hususan wanawake, vijana, na Watu wenye Ulemavu ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Waziri Ridhiwani alishukuru wadau kwa ushirikiano wao katika uandaaji wa miongozo na mifumo hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mary Maganga amesema kazi ya uandaaji wa miongozo na mifumo hiyo ilikuwa shirikishi ambapo wadau mbalimbali wa maendeleo walishirikishwa ikiwemo Shirika la Kazi Duniani (ILO), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) na Chama cha Mawakala Binafsi wa Ajira (TRAA).

Mwakilishi wa Katibu Mkuu TUCTA Rashid Mtima alisema wafanyakazi wa Tanzania wanayo imani na Serikali ya Awamu ya Sita kutokana na maboresho ya msharaha mwaka huu 2025 ambapo ulipanda kwa asilimia 35 hatua inayowafanya waende kifua mbele kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29 .

Naye Patricia Shao Mwenyekiti wa Chama cha Waajili Tanzania (ATE) alisema chama hicho kitaendelea kushirikiana na wadau wa utatu ambao ni serikali ,waajili na wafanyakazi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na nguvu kazi bora itakayochangia tija ambapo miongozo iliyozinduliwa inalenga kufika huko.