Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo amewataka wajumbe wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kusimamia uadilifu kama nguzo ya msingi katika uongozi wao.
Amesema uadilifu ndiyo msingi wa kusimamia taasisi za umma na kwamba bila uadilifu, jitihada zote za kuimarisha biashara haziwezi kufanikisha malengo makubwa ya Serikali.
Jafo amesema bila uadilifu taasisi za umma hushindwa kufanikisha majukumu yake, hivyo wajumbe hao wanapaswa kuhakikisha TanTrade inasimamiwa kwa uwazi, weledi na nidhamu ili kuleta matokeo chanya kwa taifa.
Akizungumza leo Agosti 22, 2025 wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo, Jafo bodi hiyo imepewa dhamana kubwa ya kusimamia mikakati ya kibiashara, ikiwemo kuimarisha maonyesho ya kimataifa ya biashara ya Dar es Salaam (DITF – Sabasaba) na kuiweka Tanzania katika ramani ya ushindani wa kikanda na kimataifa.
“Ndiyo maana nasisitiza, kazi ya kwanza ya bodi hii ni kuhakikisha Tantrade inasimamiwa kwa uadilifu. Pale ambapo viongozi wanashindwa kudumisha heshima na uadilifu, hata jitihada kubwa hufutika,” amesema Dk Jafo.
Hata hivyo, Jafo amesema Serikali imewekeza nguvu kubwa katika sekta ya viwanda na biashara, hivyo Tantrade ni chombo muhimu kitakachosaidia kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania.
“Tunataka kuona Tantrade ikisaidia bidhaa zetu kuingia katika masoko ya Afrika Mashariki, Afrika kwa ujumla na hata kwenye nchi za Mashariki ya Kati kama Saudi Arabia. Bodi hii lazima iwe na dira ya kuhakikisha Tanzania inanufaika na mikataba ya kibiashara tuliyo nayo,” amesema.
Ametaja sekta ya kilimo kuwa na fursa kubwa ya kuwanufaisha wakulima iwapo Tantrade itasimamia vizuri jitihada za kutafuta masoko mapya ya kahawa, korosho, chai na mazao mengine.
Pia, amewataka wajumbe wa bodi hiyo kushirikiana na timu ya watendaji wa Tantrade kwa karibu, kuhakikisha kila mkakati unatekelezwa kwa ufanisi na kusimamiwa kitaalamu.
“Mmekabidhiwa dhamana kubwa. Hakikisheni Tantrade inakuwa chombo cha mfano kwa kusimamia mikakati ya biashara kwa njia ya uwazi, nidhamu na weledi. Serikali inategemea matokeo chanya yatakayowanufaisha wafanyabiashara wakubwa na wadogo.”
Aidha, aliwataka wajumbe wa bodi kuhakikisha wanapima kwa kina changamoto zinazokabili mamlaka hiyo na kuja na suluhisho la kudumu, hususani katika maeneo ya kukuza ushiriki wa wafanyabiashara wadogo katika maonyesho ya kimataifa.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah ameeleza kuhusu umuhimu wa uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa kila hatua inapaswa kufanywa kwa uwazi na ufanisi.
Amesema kuwa bodi ni mkono muhimu wa serikali na ina jukumu la kuhakikisha mipango ya maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara inafanikishwa.
“Uwajibikaji wenu ni msingi wa mafanikio ya Tantrade. Kila mmoja lazima achukue jukumu lake kikamilifu, kuhakikisha malengo ya sekta yanatimizwa kwa ufanisi,” amesema Dk Abdallah .
Aidha, alisisitiza kuwa uwajibikaji hauhusishi tu utekelezaji wa majukumu ya kila siku, bali pia kubeba matokeo ya maamuzi yote ya bodi, kuhakikisha fedha zinatumika kwa uangalifu na huduma kwa wateja inaboreshwa kwa kiwango cha juu.
Katibu aliwataka wajumbe kuzingatia umuhimu wa uwazi, uwajibikaji wa kifedha, na ufanisi katika kazi zao, huku akisisitiza kuwa bodi mpya ni fursa ya kuhakikisha sekta ya viwanda na biashara inakua kwa kasi na inaendelea kutoa mchango chanya kwa uchumi wa Taifa.
“Tunategemea kila mmoja wenu kutumia nafasi hii kwa uangalifu mkubwa. Uwajibikaji wenu sio chaguo bali ni jukumu la lazima,”
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Ulingeta Mbamba amesema watasimamia mifumo ya taarifa ya biashara, mafunzo kwa wajasiriamali wadogo na wakati, upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi, ushirikiano wa kibiashara, matumizi ya nembo ya bidhaa na utengenezaji wa uwanja wa maonyesho wa kimataifa na .
“Kwa niaba ya wajumbe wenzangu wa bodi tunahakikisha tutaendesha majukumu yetu kwa ufanisi mkubwa ili kuchangia katika maendeleo ya biashara nchini na taifa letu kwa ujumla,” amesema Profesa Mbamba.
Mbali na mwenyekiti bodi hiyo inawajumbe wengine nane ambao ni Fred Ngajiro (Fred Vunjabei), Ahmed Yussuf, Dk Hanufa Yusuph Mohamed, Najma Hussein, Radhia Tambwe, Laiton Ernesta, Happy Kitingati na Khamis Ahmad.