Elimu, uwekezaji vikwazo ufikiaji fursa uchumi wa buluu

Dar es Salaam. Kukosekana kwa elimu ya kutosha na uwekezaji zimetajwa kuwa sababu zinazofifisha jitihada za ufikiaji wa fursa zilizopo katika uchumi wa buluu nchini.

Hayo yanasemwa wakati ambao tayari Serikali imezindua mkakati wa kitaifa unaolenga kuhakikisha fursa zilizopo katika uchumi wa buluu zinafikiwa kikamilifu.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Chuo cha Bahari (DMI), Profesa Tumaini Gurumo wakati akielezea kongamano la tatu la Kimataifa la Uchumi wa Buluu linalotarajiwa kufanyika Septemba 10 na 11  jijini hapa likibebwa na kauli mbiu isemayo “Bahari yetu, fursa yetu, wajibu wetu”.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Agosti 22, 2025 inasema uwepo wa kongamano hilo ni moja ya njia inayolenga kuhakikisha fursa zilizopo katika uchumi wa buluu zinafikiwa kimalifu.

“Uwepo kongamano hili unalenga kuwafanya watu wajue kuwa kuna fursa na kupata namna ya kuzifikia. Tunaendelea kutoa elimu ili tuweze kutatua changamoto hii ya kushindwa kutambulika kwa uchumi wa buluu kwa kufanya makongamano na kozi mbalimbali ambazo zinanzishwa katika chuo cha DMI,” amesema.

Amesema elimu hiyo imekuwa ikienda sambamba na kuwajengea watu ujuzi unaohitajika kwani ndiyo utakaowawezesha kuona matunda ya moja kwa moja.

Kuhusu uwekezaji, Profesa Gurumo amesema ni moja ya eneo linalopaswa kuangaliwa na sekta binafsi ili iweze kushiriki kimalifu na kuleta tija katika kipato cha nchi.

“Uwekezaji ni wa pande zote ukizitazama uchumi wa buluu ukizitazama Serikali itafanya kwa nafasi yake na sekta binafsi kwa sehemu yake,” amesema.

Amesema Tanzania ina pwani ya Bahari ya Hindi ya kilomita 1,400 na eneo maalumu la uchumi wa buluu la talkribani kilomita za mraba 225,000 jambo ambalo linaiweka nchini kuwa kinara katika utumiaji wa fursa hizo Afrika.

Pia, Profesa Gurumo amesema licha ya changamoto zinazofifisha kufikia kikamilifu fursa hizo, lakini uwepo wa ofisi maalumu ndani inayoshughulikia sekta hiyo ni hatua muhimu.

“Hii itafanya uchumi wa buluu kuwa na mchango mkubwa kwani kutakuwa na uratibu wa moja kwa moja unaoenda sambamba na usimamizi wa sera iliyopo,” amesema.

Baadhi ya fursa zinazopatikana kwenye uchumi wa bahari (uchumi wa buluu) ni pamoja na uvuvi wa kisasa, utalii, usafirishaji, mafuta na gesi, madini.

Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na watu kutoka taasisi zaidi ya 150, taasisi za kifedha, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na wananchi jambo litakalojenga mjadala jumuishi.

Naibu katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Abdalah Hassan Mitawi amesema kongamano hilo ni moja ya eneo ambalo litatumika katika kutafsiri mchango wa uchumi wa buluu katika Dira 2050.