BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini Kareem Mandonga sambamba na wenzao wamepimwa uzito leo kwa ajili ya mapambano yatakayofanyika kesho Jumamosi, huku bondia huyo akitamba na ngumi mpya iitwayo ‘Kusanyakusanya’.
Mandonga na wenzao wanatarajia kupigana kesho usiku katika ‘Usiku wa Mabingwa wa Tabora’ ambapo Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Belti Wella kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Tabora, Paul Matiko Chacha.
DC Upendo leo amemkambidhi bondia Abdul Zugo kitita cha Shilingi 10 milioni kama sehemu ya hamasa kwa bondia huyo ambaye atashuka ulingoni hapo kesho kupigana na Sameer Kumar kutoka India kuwania ubingwa wa Dunia wa WPBF katika uzito wa kilo 63 (Super light).
Mbali na pambano la Zugo, jukwaa hilo litasheheni mapambano mengine ya utangulizi, likiwemo Kareem Mandonga ‘Mtu Kazi’ kutoka Morogoro na Juma Farhan wa Tabora miongoni pambano ambalo pia linaamsha shangwe la mashabiki wa mchezo huo huku tambo za mabondia zikishamiri.
Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania(TPBC), Jackob Mbuya amesema maandalizi ya mapambano hayo yamekamilika kwa kukidhi vigezo vyote stahiki.
Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Tabora kuwa mwenyeji wa ngumi za kiwango cha dunia ambapo mashabiki walishuhudia mabondia hao wakitupiana maneno ya tambo wakati wakifanya face off mara baada ya kupima uzito na afya
Mandonga alitamba ameenda Tabora kutambulisha ngumi mpya iitwayo ‘Makusanyakusanya’.