Shinyanga. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa viongozi wa Serikali waliopo maeneo ya ajali ya mgodini kushiriki taratibu zote za mazishi kwa watu waliofariki ajali ya mgodini na kuwasilisha rambirambi zake.
Akizungumza leo Agosti 22, 2025 na viongozi pamoja na waathirika wa ajali ya mgodini katika eneo la tukio la ajali ya mgodi unaomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi uliopo kijiji cha Mwongozo kata ya Mwenge Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, pia amewasilisha salamu za pole kwa wananchi hao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita kabla ya kushiriki zoezi la kuwaokoa waliokwama ardhini.
“Rais Samia ameniagiza kuwafikishia salamu za pole na rambirambi pia kanituma kuleta maagizo kwa viongozi wa Serikali waliopo eneo hili kuhakikisha wanahudhuria misiba yote ya watu waliopoteza maisha katika ajali hii na kuwakilisha rambirambi alizotoa katika familia hizo” amesema Lukuvi.
Maagizo ya viongozi wa Mkoa
Agosti 16, 2025 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro alitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dk Kalekwa Kasanga kufanya utaratibu wa kuweka ofisi ya muda ya mtendaji wa kijiji katika eneo la tukio la ajali ambayo itatumika kuwasajili wageni waliokuja kusubiri ndugu zao kwa ajili ya kuhudumiwa na serikali.

Agosti 18, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita alitoa maelekezo kwa familia zilizokuja kusubiri ndugu zao, kuchagua wawakilishi wawili au watatu ambao watabaki ili iwe rahisi kwa serikali kuhudumia familia hizo kwa sababu isingependa kuona watu wanapata changamoto ya mahitaji maalum wakati tayari wako kwenye huzuni.
Ikumbukwe kuwa ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 wakati maduara ya mgodi huo yakiwa yanafanyiwa ukarabati na kupelekea mgodi kutitia na kufukia watu 25, Agosti 12, 2025 watu watatu waliokolewa wakiwa hai na kukimbizwa hospitalini kwa huduma ya kwanza, wawili wameruhusiwa lakini mmoja alipewa rufaa ya kwenda Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.
Agosti 13, 2025 mtu mmoja aliokolewa akiwa ni majeruhi na alipelekwa hospitalini lakini alifariki wakati anapatiwa matibabu. Juhudi za kuokoa ziliendelea na Agosti 15 mwili wa mtu mmoja uliopolewa huku Agosti 16, 2025 watu wawili waligundulika walipo eneo la ardhini na Agosti 17, 2025 watu hao watolewa wakiwa wamekufa.
Pia, Agosti 19 mtu mmoja alitolewa akiwa amepoteza maisha na Agosti 21, 2025 miili ya watu wawili ilitolewa, juhudi za kuwatafuta wengine ziliendelea kwa kasi kuwatafuta wengine 15 waliokuwa wamebaki huku familia zao zikisubiri na kuwepewa mahitaji yote muhimu na serikali.
Hadi sasa watu 11 wametolewa huku watatu wakiwa hai na wanane wakiwa wamefariki, juhudi za kuendelea kuwatafuta wengine 14 zinaendelea kwa kasi kwa kutumia mashine za utambuzi wa ardhini kujua maeneo waliopo.