‎‎Aliyedaiwa kumuua mumewe afariki dunia baada ya kunywa sumu

‎Mufindi. Elizabeth Kihombo (46), mkazi wa Kijiji cha Ihefu kilichopo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, aliyekuwa anatuhumiwa kwa kumuua mume wake, Philimon Lalika (49), amefariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibubu katika Hospitali ya Mji wa Mafinga.

‎Tukio hilo limetokea Agosti 20, 2025 katika Kijiji cha Ihefu ambapo Elizabeth alimuua mume wake kwa kumchoma na kisu tumboni kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ugomvi uliotokana na wivu wa kimapenzi.

‎Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi, marehemu akiwa amelala na mke wake, ulitokea ugomvi uliosababisha mtuhumiwa kutenda kosa hilo ambapo baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alijaribu kunywa dawa ya kuhifadhia nafaka kwa lengo la kujiua.

‎Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 22, 2025, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Mafinga, Dk Victor Msafiri amethibitisha kutokea kwa kifo cha Elizabeti wakati akiendelea kupatiwa matibau katika hospitali hiyo.

‎Amesema Elizabeth alipokelewa hospitalini hapo saa 11 alfajiri akitokea katika Kituo cha Afya cha Mdambulo ambako alikuwa anapatiwa matibabu hayo.

‎Dk Msafiri ametoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi, badala yake washirikishe wataalumu wa masuala ya afya ya akili pamoja na Jeshi la Polisi ili liwasaidie katika changamoto zinazowasumbu kabla madhara hayajatokea.

‎Awali akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihefu, kata ya Mdabulo, Chesco Mhwagila amesema tayari mwili wa mwanamke huyo umezikwa kijijini hapo.

‎Wakati wakiendelea na mazishi ya Elizabeth, amesema viongozi pamoja na madhehebu ya dini wameelendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuacha kujichukulia sheria mkononi na endapo kama watakuwa na shida katika uhusiano basi watafute viongozi dini au vyombo vya sheria ili kusuluhisha.

‎“Inawezekana Elizabeth alikuwa na changamoto ambayo anapitia bila kusema, matokeo yake anaweka vitu moyoni, madhara yake ndio kama haya, hivyo niwasihi wananchi, viongozi tupo kwa ajili yenu mkiwa na changomoto tuleteeni,” amesema Mhwagila.

Kwa kufanya hivyo, amesema matukio ya ajabu kama hayo yatapotea kwani yanaacha watoto, hali ambayo inasababu kuathirika kisaikolojia.

Mwenyekiti huyo amesema Elizabeth pamoja na mume wake, Lalika wameacha watoto 11.