Utata urais wa Mpina, Msajili kuwakutanisha ACT-Wazalendo, Monalisa leo

Dar es Salaam. Sakata la urais wa Luhaga Mpina ndani ya Chama cha ACT-Wazalendo limechukua sura mpya, baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kuziita mezani pande mbili zinazosigana leo Jumamosi, Agosti 23, 2025.

Agosti 6, 2025, mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo ulimchagua Mpina kuwa mtiania wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Tayari Mpina, aliyewahi kuwa mbunge wa Kisesa (CCM), mkoani Simiyu na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, amekwisha kabidhiwa fomu na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.

Wakati Mpina akiendelea kutafuga wadhamini 200 katika kila mkoa kwenye mikoa 10 ikiwemo miwili ya Zanzibar, Katibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala aliibua malalamiko kwamba Mpina amepitishwa kinyume cha kanuni za uendeshaji wa chama hicho.

Monalisa alidai uteuzi wa Mpina haukufuata masharti ya kanuni za chama, hususan kifungu cha 16(4)(i, iii, na iv) cha toleo la mwaka 2015, kinachosema mgombea urais lazima awe mwanachama wa chama hicho kwa angalau mwezi mmoja kabla ya uteuzi rasmi.

Monalisa amedai Mpina alijiunga na chama hicho Agosti 5, 2025, na kuteuliwa kuwa mgombea urais siku iliyofuata, Agosti 6, 2025. Hatua anayodai, inakiuka masharti ya chama na inatoa picha ya kuvunjwa kwa taratibu za ndani za uendeshaji wa chama hicho.

Monalisa alifikisha malalamiko yake kwa Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo. Baada ya siku kadhaa, akafikisha suala hilo ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ambayo nayo iliiandikia barua ACT-Wazalendo kutaka majibu ya malalamiko ya Monalisa.

Baada ya ACT-Wazalendo kujibu. Ofisi ya Msajili iliyawasilisha kwa Monalisa Agosti 21, 2025. Hata hivyo Monalisa hakuridhika nayo na kumwandikia tena barua msajili kuomba hatua zikuchuliwe kwani chama chake kimeshindwa kujibu hoja zake.

Jana Ijumaa, Agosti 22, 2025, akizungumza na Mwananchi, Msajili Msaidizi wa Vyama Vya siasa, Sisty Nyahoza amesema wamepokea barua ya Monalisa:”Na leo saa 5:00 asubuhi tumewaita waje tusikilize pande zote mbili na baada ya kuwasikiliza tutatoa uamuzi.”

Alipoulizwa uamuzi utatoka leo hii hii, Nyahoza amesema:”Tutajipa muda kuchambua mawasilisho waliyotuletea na maelezo waliyoyatoa lakini itakuwa ni haraka kabla ya Agosti 27 kwani tukizidisha hapo itakuwa haina maana.” amesema.

Baada ya maelezo hayo, Mwananchi limezungumza na Monalisa kujua kama amepata taarifa ya wito huo, amekiri kupokea wito huo huku akisisitiza majibu yaliyotolewa na chama chake hajaridhishwa nayo.

“Kesho nitaenda Ofisi za Msajili, sitakuwa peke yangu nitaambatana na mawakili wangu watatu kwenda kukisikiliza chama kuhusu malalamiko yangu tukiwa na Msajili,” amesema Monalisa.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo-Bara, Isihaka Mchinjita amekiri kupokea wito kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Tumepokea huo wito wa kesho (leo) ofisini kwake. Ingawa ujumbe huu unahusisha ofisi ya Katibu Mkuu, endapo atakuwa na nafasi, anaweza kujitokeza kwa ajili ya mazungumzo zaidi,” amesema Mchinjita.

Mwananchi limemtafuta Mchinjita baada ya Katibu Mkuu, Ado Shaibu simu yake kuita pasi na kupokelewa.