WATETEZI wa Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la FA, Yanga ni kama wameshamaliza usajili wa kikosi kwa ajili ya hesabu mpya za msimu ujao kwa kumuongezea beki wa kati, Frank Assinki, lakini ndani ya ujio wa kitasa hicho raia wa Ghana kuna vita tano nzito.
Vita hizo mpya zilizoibuliwa ndani ya Yanga zitaamuliwa na kocha Romain Folz na wasaidizi wake ambao wanaendelea kunoa makali katika kambi ya timu hiyo iliyopo Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Hadi sasa katika dirisha hili la usajili, Yanga rasmi imewaongeza wachezaji 10 wakiwamo sita wa kigeni na wazawa wanne wakiwamo mabeki, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Frank Assinki.
Wengine ni viungo Abubakar Nizar ‘Ninju’, Abdulnassir Mohammed ‘Casemiro’, Offen Chikola, Mousa Balla Conte, Lassine Kouma, Celestin Ecua, Mohamed Doumbia na straika Andy Boyeli.
Ujio wa mastaa hao 10 umezusha vita tano ngumu ambazo zimetoka katika nafasi tano tofauti ndani ya kikosi hicho, hali inayowaongezea presha mastaa hao katika kuwania nafasi ndani ya kikosi hicho cha Folz.
Folz hakuwa na Yanga msimu uliopita ambapo maboresho ya kikosi hicho yataifanya Yanga kama kuanza upya chini ya Mfaransa huyo, kwa kuanza hesabu za kuunda kikosi chake cha kwanza na hapo ndipo kutakoleza vita hiyo.
Tuanze na kuangalia pale beki wa kushoto, ambapo kuna majina mawili tu Chadrack Boka aliyeletewa mtu wa kazi, Tshabalala ambaye hana rekodi ya kukaa nje kwa majeraha, wawili hao watakuwa wanawania nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.
Kama Boka atakuwa sawa kiafya, lazima atajipanga kuhakikisdha Tshabalala hamuondoi katika hesabu za Folz, lakini haitakuwa rahisi kwa Tshabalala kuja kulikubali benchi akiwa na timu hiyo mpya, iliyomnyakua baada ya kumaliza mkataba mitaa ya Msimbazi.
Nafasi ya beki wa kati kwa misimu karibu minne sasa, imekuwa chini ya nahodha msaidizi Dickson Job na Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, huku nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto akisotea benchi na sasa ameongezwa Assinki.
Ujio wa Assinki sio taarifa njema kwa Bacca wala Job ambapo beki huyo raia wa Ghana juzi tu alipoanza mazoezi baada ya utambulisho, ameonyesha yeye ni ‘askari’ mwingine mzito katika ukuta wa mabingwa hao.
Assinki anaweza kuhatarisha pacha ya Bacca na Job, lakini itawaongezea presha wawili hao kufanya mambo kwa umakini, wakijua kosa moja tu linaweza kumuondoa mmoja wapo, hasa ukizingatia eneo hilo sio rahisi kuwa na mabadiliko mara kwa mara kutokana na kuhitaji watu wanaoweza kucheza kwa kuelewana.
Pale namba sita nako kutakuwa na vita ya aina yake. Kwa ambaye hajaona mazoezi ya Yanga ni rahisi kwake kupiga hesabu za haraka kwamba hapo atacheza Conte na Mudathir Yahya, lakini ukiona kazi ya Casemiro utakutana na kigugumizi.
Ubora wa Casemiro kwa anachofanya mazoezini, akija kuhamishia uwanjani kwenye mechi za timu hiyo kisha akafanya kwa muendelezo lolote linaweza kutokea kwa Mudathir au hata Conte.
Casemiro anapokonya mipira, lakini kama haitoshi anasogeza timu mbele kwa kubadilika haraka sehemu ya kuanzisha mashambulizi, wakati akiwa na mpira.
Balaa walilofanya Clement Mzize na Prince Dube msimu uliopita wawili hao waliitengenezea timu hiyo jumla ya mabao 27 ambapo sasa wanakwenda kwenye msimu mwingine wakiongezewa mtu mmoja aliyeanza na salamu ya mabao.
Mzize ndiye mfungaji bora msimu uliopita ndani ya timu hiyo akifunga mabao 14. Kama hatauzwa ina maana atabaki kuendelea kufunga mabao sawa na Dube aliyefunga 13, lakini Boyeli katika mchezo wa kwanza wa kirafiki kule Rwanda akaweka kambani bao lake la kwanza.
Kama haitoshi Boyeli huko mazoezini Yanga anavuruga vibaya makipa wa timu hiyo, muulize Djigui Diarra alichofanyiwa juzi pale Avic Town, alipofungwa bao moja la kikatili, lakini Dube naye anaendelea na alipoishia, nani ataanza hapo hilo ni swali litamsubiri Folz na wasaidizi wake.
Vita ngumu na kubwa zaidi itakuwa pale nafasi ya kiungo mshambuliaji yaani namba 10, hapo kutakuwa na mambo mazito, kwani kuna mashine sita zitapigania ufalme.
Hebu cheki, hapo kuna Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Ecua, Doumbia na Kouma hawa wote wanatakiwa kwanza kujichuja kwenye nafasi hii kabla ya kutafutiwa maeneo mengine.
Kumbuka ndani ya misimu mitatu nafasi hii ilikuwa chini ya Stephanie Azizi KI aliyeuzwa kule Wydad Athletic ya Morocco, msimu huu inatafuta mtu mpya wa kuimiliki.
Hesabu zinambeba Zouzoua, lakini wenzake watano waliosalia nao wanajua vyema kuitumikia nafasi hiyo kwa utumishi mzuri hatua ambayo itahitaji muda kuamua nani atamkosha Folz.
Kocha Folz akizungumzia ushindani huo wa nafasi hizo ameliambia Mwanaspoti kuwa: ”Kila mchezaji ana nafasi ya kutafuta nafasi ya kucheza, tuna wachezaji wengi bora kwenye kikosi chetu.”
“Kwa wakati kama huu sisi makocha tunapata nafasi ya kuangalia nani anaweza kutumika wapi, sidhani kama ni kazi ngumu sana lakini tunatarajia kuwa na timu nzuri kwa msimu ujao,”
alisisitiza kocha huyo aliyetua akitoka Afrika Kusini kumpokea, Miloud Hamdi aliyeenda Misri.