Kiungo Kagera ajitabiria Coastal | Mwanaspoti

KIUNGO mkabaji mpya wa Coastal Union, Geofrey Manyasi amesema anaamini msimu huu utakuwa mzuri kwa wana Mangushi na hayatomkuta yaliyomtokea msimu uliopita akiwa na Kagera Sugar.

Manyasi amejiunga na Coastal katika dirisha kubwa la usajili msimu huu lililofunguliwa Agosti 15, 2025, akitokea Kagera Sugar iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliopita.

Nyota huyo wa zamani wa Boma, Pamba, Tanzania Prisons na Geita Gold, imekuwa na bahati mbaya kwa misimu miwili mfululizo akishuka daraja na Geita Gold na Kagera Sugar, jambo ambalo anaamini msimu huu ataliepuka.

Manyasi ni miongoni mwa sajili mpya zilizofanywa na Coastal Union ambayo imefanya mabadiliko makubwa ya kikosi ilianza na benchi la ufundi kwa kumleta kocha mkuu, Alli Mohamed Ameir na msaidizi wake, Bakari Mngazija.

Pia imesafisha kikosi kwa kuachana na wachezaji wake, Lameck Lawi, Aaron Kalambo, Abdallah Denis, Daud Semfuko, Lucas Kikoti, Miraji Abdallah, Sabri Kondo na Msekeni Athumani.

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu usajili huo, Manyasi alisema baada ya kucheza muda mrefu katika timu za mikoa ya Kanda ya Ziwa yeye na menejimenti yake wameona kwa sasa wabadilishe mazingira kwa kujiunga na Coastal Union ya Tanga.

”Nipo Tanga huku sasa hivi nimesaini Coastal Union, nimeona nibadili mazingira tena, nilitafutwa na timu kadhaa zikiwemo KMC, Mtibwa Sugar na Singida Black Stars lakini menejimenti imeona nije Coastal Union,” alisema Manyasi na kuongeza;

“Pia conditions (vigezo) zao sio mbaya sana. Nimejiandaa vizuri tu na naamini utaenda kuwa msimu mzuri sana kwangu huu, nawaomba mashabiki waendelee kutarajia yale mazuri waliyoyazoea kwangu.”