MECHI mbili za robo fainali za michuano ya CHAN 2024 zimepigwa jana Ijumaa na leo zinapigwa nyingine za mwisho ili kujua timu zitakazoumana katika nusu fainali, lakini kuna kazi inaendelea kwenye michuano hiyo wakati wachezaji wa timu shiriki wakipambana kuwania tuzo za msimu huu.
Kabla ya mechi za jana tayari mabao 74 kutoka kwa wachezaji 62 yalikuwa yametinga wavuni kupitia mechi za makundi zilizomalizika mwanzoni mwa wiki yakiwamo mawili ya kujifunga na jumla ya penalti 11 kati ya 12 zilizopigwa, baada ya moja kukoswa na Allain Okello wa Uganda The Cranes.
Mabao hayo 74 yamepatikana kupitia mechi 36 zilizopigwa katika hatua ya makundi iliyoshirikisha jumla ya timu za nchi 19 ambapo 11 ziliaga na kuziacha nane zilizotinga robo fainali ambapo jana wenyeji Tanzania walikuwa na kibarua mbele ya Morocco, huku Kenya wakiumana na Madagascar.
Rekodi zinaonyesha wachezaji 60 wamehusika kufunga mabao 72, huku wawili Quinito (Angola) na Leonard Ngenge(Nigeria) wakijifunga.
Hii ni tofauti na msimu uliopita wa mwaka 2022 ambapo zilichezwa jumla ya mechi 29 na kufungwa mabao 55 tu, yakiwamo manne ya kujifunga.
Katika orodha ya wafungaji wa fainali hizi za 2024 ambazo ni za nane, wachezaji watatu ndio vinara kila mmoja akifunga mabao matatu ambao ni Oussama Lamlioui wa Morocco, Allan Okello wa Uganda na Thabito Kutumel wa Afrika Kusini ambao wanafuatiwa na wengine wanane wenye mabao mawili kila mmoja.
Nyota hao wenye mabao mawili kila mmoja ni; pamoja Clement Mzize (Tanzania), Austin Odhiambo (Kenya), João Manha ‘Kaporal’ (Angola), Abdelrazig Omer (Sudan), Lalaina Rafanomezantsoa (Madagascar), Japhte Kitambala (DR Congo), Mohamed Hrimat (Morocco) na Mkenya Ryan Ogam.
Nyuma ya nyota hao kuna wachezaji wengine 41 waliofunga bao moja kila mmoja (orodha hii ni kabla ya mechi za jana za robo fainali).
Nyota hao 60 wenye mabao katika msimu huu hususani wale wanaoongoza orodha na mabao matatu kila mmoja wana kazi ya kuwania tuzo ya Mfungaji Bora kwa michuano ya mwaka huu, ili kuona kama wanaweza kupiku rekodi ya msimu uliopita ambao Aymen Mahious wa Algeria alikuwa kinara na mabao matano kama ilivyokuwa kwa Soufiane Rahimi wa Morocco aliyetwaa kiatu fainali za 2020.
Hadi sasa rekodi ya mfungaji bora mwenye mabao mengi, inashikiliwa na Ayoub El Kaabi wa Morocco aliyetwaa tuzo akiwa na mabao tisa katika fainali za mwaka 2018, ikiwa ndiye mfungaji bora wa muda wote hadi sasa, kwani hakuna mchezaji aliyewahi kufunga idadi hiyo katika fainali moja.
Mbali tuzo ya mfungaji bora wa 2024, lakini fainali za mwaka huu zilizoandaliwa kwa pamoja na mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda, pia kuna vita ya tuzo ya kipa bora, mchezaji bora na hata kocha bora ambapo kwa msimu uliopita ambao Senegal ilibebea ubingwa tuzo ziligawanyika.
Kwa upande wa Kipa Bora kwa msimu uliopita tuzo ilienda kwa kipa wa Senegal, Pape Sy wakati ile ya Mchezaji Bora ilibebwa na Houssem Eddine Mrezigue wa Algeria, ilihali Kocha Bora alikuwa ni; Pape Bouna Thiaw wa Senegal aliyeiwezesha nchi hiyo kutwaa ubingwa wa kwanza wa fainali hizo.
Michuano ya mwaka huu iliyoanza Agosti 2 itafikia tamati Agosti 30 kwa kupigwa mechi ya fainali jijini Nairobi, Kenya ili kujua nyota gani na timu zipi zitakazoibuka kidedea kwa kubeba tuzo za msimu huu ikiwamo ya timu yenye mchezaji wa kiungwana ambayo 2022 ilibebwa na Senegal.