Dar es Salaam. Miaka 15 iliyopita, kupata ugonjwa wa moyo nchini Tanzania kulikuwa ni kama hukumu iliyoambatana na gharama kubwa kifedha, safari ndefu kwenda nje ya nchi au kukata tamaa ya matibabu na kupona.
Kabla ya mwaka 2008, upasuaji mkubwa wa moyo haukufanyika nchini, hivyo iliwalazimu wagonjwa kusafiri hadi India na mataifa mengine kupata tiba; kwa wengi safari hiyo haikuwezekana.
Hatua za kuijengea nchi uwezo wa kutoa tiba za moyo zilianza kubadilisha hali hiyo, leo hii mabadiliko hayo yametengeneza mapinduzi yanayookoa maisha na fedha kwa wengi.

Madaktari bingwa wa moyo wa watoto wa JKCI wakifanya upasuaji wa kufunga tundu la moyo la mtoto bila kufungua kifua. Utaratibu huu hufanywa kupitia chale ndogo kwenye paja kwa msaada wa Cathlab (Catheterization laboratory).
“Nilikuwa sijui kama huduma zinapatikana Tanzania,” anakumbuka Sarah Jackson, mkazi wa Kivule, Dar es Salaam aliyegundulika kuwa na tatizo la moyo mwaka 2016 na kuanza tiba katika hospitali binafsi. Daktari aliposhauri afanyiwe upasuaji, alilazimika kwenda India.
“Safari iligharimu zaidi ya Sh20 milioni, mume wangu alinisaidia tukaenda,” anasema Sarah ambaye ni ofisa wa Jeshi la Polisi nchini.
Anasema walitakiwa kurudi India baada ya miezi sita lakini hakufanya hivyo ila alihudhuria kliniki katika hospitali za ndani.
Wagonjwa wa moyo wasimulia masaibu wanayokumbana nayo
Mwaka 2019 hali yake ilizorota, daktari alishauri apelekwe Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akiwa hapo alishangazwa kwamba upasuaji aliofanyiwa India unafanyika pia nchini na bima yake ya afya iligharimia.
“Nilikuwa nikipatwa kizunguzungu na kupoteza fahamu mara kwa mara. Baada ya upasuaji mwingine JKCI, najihisi kama mtu mpya. Sikutakiwa hata kurudi India kama walivyoshauri awali,” anasema.
Kwa upande wake, Oswald Mollel, mkazi wa Arusha anasema alihudumiwa katika taasisi hiyo mwaka 2009 baada ya kuhangaika ndani na nje ya nchi bila mafanikio.
“Sikutarajia ningeishi mpaka leo,” anasema Mollel, akieleza tatizo lake ni kusinyaa kwa mishipa ya moyo na kuna wakati ilifunga kiasi cha kushindwa kusukuma damu.
Kutokana na hali hiyo, anasema alitafuta huduma ndani na nje ya nchi, lakini ukubwa wa gharama ukasababisha ashindwe kupata tiba.
“Kenya walitaka nilipe Sh300, 000 za Kenya (zaidi ya Sh5.9 milioni za Tanzania) hiyo ilikuwa mwaka 2007, sikuwa na fedha nilirudi Tanzania,” anasema.

Dk Peter Kisenge, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI.
Anasema akiwa nchini alianza mchakato wa kutafuta ufadhili ili kwenda India, ndipo mwaka 2009 alipopata taarifa kuhusu huduma hizo kutolewa kwenye kitengo cha upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Anasema alianza matibabu hapo mwaka 2009 hadi 2011 akapona, kilichobaki ni kwenda kliniki kuangalia afya yake.
“Kwa sasa ninakwenda kliniki mara moja kwa mwaka, sikujua kama ningepona maana sikuwa na uwezo binafsi wa kwenda India wala Kenya, gharama zilinishinda,” anasema.
Anasema alikuwa miongoni mwa wagonjwa wa mwanzo JKCI, hivyo hakulipa gharama ya matibabu zaidi ya nauli ya kutoka Arusha anakoishi kwenda hospitali Dar es Salaam.
Simulizi za Sarah na Mollel zinaakisi mabadiliko katika mfumo wa afya nchini yaliyoanza mwaka 2008 kwa kuanzishwa kitengo cha upasuaji wa moyo MNH, hatua iliyopandikiza mbegu za kuundwa kwa JKCI, taasisi iliyozinduliwa mwaka 2015 kama chombo cha umma, kikibobea katika huduma za moyo.
Dk Evarist Nyawawa, Mkuu wa Idara ya upasuaji wa moyo kwa watu wazima JKCI, anasema hatua kubwa ya kujitegemea ilikuja baada ya madaktari wa Kitanzania kurejea kutoka mafunzo India na Israel, wakiwa na ujuzi wa kuokoa maisha uliokuwa haupatikani nchini kabla.

“Tunatibu mishipa iliyopanuka, valvu zilizoharibika na mishipa iliyoziba. Tulianza kwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa 105 kwa mwaka, hasa kwa matatizo ya kuzaliwa nayo na valvu kuharibika. Sasa tunafanya upasuaji kwa zaidi ya watu 800 kwa mwaka, ikiwemo operesheni ngumu kama kubadilisha mishipa na valvu za moyo,” anasema.
Anasema gharama za wastani na upatikanaji wa huduma JKCI umekuwa mkombozi akitoa mfano kuwa, upasuaji wa mishipa ya moyo unaogharimu zaidi ya Sh40 milioni India, hapa nchini unafanyika kwa kati ya Sh15 milioni na Sh20 milioni, huku wagonjwa wakisaidiwa na bima za afya jambo lisilopatikana kwa urahisi nje ya nchi.
Anasema taasisi hiyo imekuwa kituo cha rufaa cha kikanda, ikipokea wagonjwa kutoka Kenya, Uganda, Zimbabwe, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
“Wagonjwa kutoka nje ya nchi hulipa gharama ya juu zaidi ya asilimia 20 hadi 30 kulingana na huduma wanazopata, ukilinganisha na wazawa,” anasema.

Anasema JKCI pia imeingia ubia na taasisi za kimataifa na kupeleka wataalamu kusaidia upasuaji wa moyo kwa watoto nchini Zambia kwa kushirikiana na madaktari kutoka Israel.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Timoth Lyanga anasema kuna uhusiano wa karibu kati ya afya na uchumi kwa kuwa ni vitu vinavyotegemeana.
Anasema huwezi kupatikana uchumi, pasi na watu wenye afya njema na hata afya haitapatikana iwapo hakutakuwa na uchumi imara.
Katika muktadha huo, anaeleza mapinduzi yaliyofanyika katika sekta ya afya yanatoa hakikisho la uponyaji wa nguvukazi au rasilimali watu na hatimaye itumike kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi.
“Ugonjwa si jambo la kukusudia, mara nyingi linatokea, kama Taifa ukiwa na uwezo wa kutibia watu wako, maana yake unainusuru rasilimali watu iendelee kusalia. Ukikosa uwezo wa kutibia utayumbisha uchumi,” anasema.

Sarah Jackson, mkazi wa Kivule jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa wagonjwa wanaopata matibabu katika JKCI.
Katika afya, anasema kuna uwezekano wa kuyumbisha uchumi, iwapo watu katika Taifa watalazimika kutumia gharama kupata huduma za matibabu nje ya nchi yao.
“Fikiria raia wako analipa Sh50 milioni kwenda nchi fulani kusafiri na kutibiwa, ile fedha umepeleka nje, yupo atakayeshindwa atapoteza maisha au akaugua maisha, unapungukiwa nguvu kazi, unabaki na watu tegemezi. Lazima uchumi uporomoke,” anasema.
Dk Lyanga anasema uwekezaji zaidi unahitajika katika sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu ndani ya Taifa lao na ziwe stahiki na zinazowasaidia.
“Akilipia huduma ndani maana yake fedha inazunguka ndani, hivyo ndivyo uchumi unavyokua. Uchumi unakua zaidi kama unapata wageni wanaokuja kutibiwa kwako kama ilivyo JKCI,” anasema.
Anasema matibabu mara nyingi huwaangusha wengi katika umasikini, lakini yakipatikana ndani yanaweza kuwa na machaguo mbalimbali, ikiwemo bima.
Kuhusu wananchi wasio na bima ya afya na wasioweza kumudu gharama, Dk Nyawawa anasema kuna mfumo wa ruzuku.

“Kwa wale wasioweza kulipa, huelekezwa kwenye dawati la ustawi wa jamii hapa (JKCI). Baada ya kuthibitishwa kweli hawawezi kumudu, hupatiwa matibabu bure,” anasema.
Amesema kwa makundi mengine, hususan watoto, taasisi hupokea msaada na michango kutoka wadau mbalimbali wakiwamo kutoka benki na taasisi binafsi.
Mwenyekiti wa Heart Team Africa Foundation (HTAF), Mussa Zungu anasema taasisi hiyo inasimamia na kuratibu jitihada za kusaidia wananchi, hususani watoto wenye matatizo ya moyo.
Zungu, anasema zaidi ya watoto 13,800 nchini huzaliwa kila mwaka wakiwa na matatizo ya moyo na familia nyingi haziwezi kumudu gharama za tiba.

Dk Evarist Nyawawa, Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Moyo kwa Watu Wazima JKCI.
“Tunatambua hili, tunalazimika kuhamasisha michango kupitia kampeni mbalimbali pamoja na msaada wa Serikali ili kuwasaidia wagonjwa hawa,” anasema akieleza mwaka 2025 wamekusanya zaidi ya Sh3.2 bilioni kusaidia huduma hizo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge katika miaka minne taasisi hiyo imetibu wagonjwa 745,837, wakiwamo watu wazima 674,653 na watoto 71,184, huku 30,645 kati yao wakihitaji kulazwa hospitalini.
Dk Kisenge ameeleza kuwa hospitali ya Upanga pekee ilihudumia wagonjwa 513,484, huku hospitali ya Dar Group iliyopo Tazara, Dar es Salaam ikihudumia wagonjwa 278,839.