Hekaya za malevi: Akili mnemba kizibo cha akili – 2

Dar es Salaam. Siwezi kubishana na umati unaodai kuwa akili mnemba ni maendeleo. Hoja yangu ni lugha inayotumika  tukisema “Maendeleo ni kutoka mahala na kwenda mahala pengine”, haimaanishi kwenda kinyumenyume ni maendeleo. Hivyo nakusudia kusema kuwa matumizi ya akili mnemba bado hayajaeleweka sawasawa miongoni mwa watumiaji wake. Wanaiweka mbele wakidhani kuwa ina silika za ufundishaji.

Hebu chukua mfano huu: Kobe na sungura walishindana mbio baada ya kutambiana ni nani mwenye kasi zaidi kuliko mwenzie. Wanyama wengine walitanda kando ya njia kushuhudia kituko kile tangu lini kobe akawa na kasi ya kumzidi hata jongoo! Mpambano ukaanza alfajiri ile huku kila mnyama akimshangilia sungura. Naye sungura alianza mbio kwa kasi akimwacha kobe akijikongoja.

Alipokwisha kukimbia umbali wa nusu uwanja, sungura alisimama na kutazama nyuma. Hakuona hata dalili ya kobe kutokeza. Akarudi nyuma kwenye mstari wa kuanzia na kumkuta kobe katika hatua zake za mwanzoni. Sungura alicheka sana, akamwambia: 

“Naenda kulala katikati ya uwanja, utanikuta pale mchana!” Baada ya kusema hivyo, sungura akakimbia nusu uwanja na kutayarisha kitanda, kisha akalala fofofo.
Baada ya muda mrefu kobe alifika eneo lile. Akampita sungura kimyakimya na kuendelea na mbio.

Mchana sungura alistushwa na mrindimo wa shangwe za wanyama. Akaamka na kuuliza kwa hamaki: “Yuko wapi huyu mwendapole?”. Wanyama wakamjibu “anavishwa taji la ushindi kule mbele!” Sungura alitoka mbio za ajabu kama risasi. Lakini haikusaidia kwani alimkuta kobe ameshamaliza akiwa mshindi.

Kwa hadithi hiyo nadhani umejifunza kuwa tunachopata kutoka kwa akili mnemba ni kasi isiyo na malengo kusudiwa. Ni lazima ujue unataka nini kabla ya kutafuta. Mtu yeyote anaponunua kompyuta anaiweka programu kwa kadiri ya mahitaji yake. Kuna watumiaji wa aina tofauti kama madaktari, wahandisi, wahasibu, wasanii, wanasheria na kadhalika. 

Daktari hawezi kutumia kompyuta ya mhasibu hadi pale atakaposomea uhasibu.  Mwanzoni tulifanya makosa kuwaelekeza watoto wetu kuiparamia elimu ya juu bila kuzingatia hii ya chini. Nadhani matokeo yale yamekuja na mapema.

Imetokea baada ya tatizo la ajira, baadhi yetu tuliwapeleka vijana huko vijijini kuangalia fursa. Tukagundua kuwa walikuwa wamepunguzwa badala ya kuongezwa akili. Tulishangazwa sana kuona mhandisi wa majengo anashindwa kukarabati nyumba ya msonge.  

Hii inatoa mwangaza wa kwamba tunasomea vitu visivyotusaidia. Mtu mwenye elimu ya juu anatakiwa kuwa msaada wa wasio na elimu kabisa. Zamani watoto walikuwa wakihitimu maneno bila kujua nini hasa wanachofundishwa. Walidhani kuitwa “Mhandisi” ni heshima tu, lakini ni afadhali sasa muunganiko wa Elimu ya Msingi na Elimu ya Ufundi. Huu utatusaidia kujua kuwa haiwezekani kupiga tofali kabla ya kujua kuchanganya udongo.

Kwa kukosa uelewa, Watanzania wengi wanadhani akili mnemba inafundisha mtu kufanya kazi. Fikra hizi zinawafanya watumiaji kuacha kujifunza stadi za kazi kwa kuitegemea akili hiyo. Hata wale walio kazini wanaacha kuboresha maujuzi yao na kufanya kazi kwa kutumia akili mnemba. Hii si sawa, kwani mambo yanayotengenezwa na wanadamu yanahesabika muda wake.

Wengine hawataki kuniamini. Lakini kwa kukuhakikishia hilo, watazame hao wanaotuundia teknolojia hizi wanavyokwenda mbele na nyuma. Wao pamoja na kuendelea kutoka usomaji wa vitabu vya kuchapwa hadi kusoma kielektroniki, wamerudia kusoma vitabu vinavyochapishwa na viwanda. Waligundua mashine za kucheza video nyumbani lakini wakarudia kwenda kwenye kumbi za sinema. Hawaitupi asili yao.

Ndio maana nasema akili mnemba ni kizibo cha akili kwa wabongo. Hivi sasa hatununui magazeti kwa kudhani kusoma mitandaoni ni maendeleo. Hatuendi uwanjani kushangilia timu ya Taifa tukidhani inatosha kuangalia kwenye TV. Yaani ni sawa na kuchana suruali zako za mtindo wa “chupa” (tinabuu) kwa kushobokea pekos. Baada ya muda “chupa” zinarudi kwa mtindo uleule zikiitwa “modo”.  

Nayafananisha ya sasa na maisha yetu ya roboti. Mwanafunzi anayekwenda kufanya utafiti, anaacha kutumia akili yake kusoma vitabu kwa kutegemea akili mnemba itamuandikia tasnifu yote. Matokeo yake, anapoulizwa maswali ya msingi darasani, anatoa macho kama kafumaniwa akichepuka na mke wa bosi wake (tena mwanajeshi). AI imemsaidia kuandika, lakini haikumsaidia kufikiri.

Ieleweke kwamba akili mnemba si jambo jipya. Wakati uliopita mtu aliyeumbwa na akili mnemba alikuwa akitumia akili yake kukumbuka nyimbo, historia na matukio muhimu. Leo, mtu anajivunia kuwa na akili mnemba ya simu yake. Lakini simu ikipotea, kumbukumbu zake hupotea pia. Tumefika mahali ambapo tunaweza kufikiri vizuri tu tukitumia mtandao. Bila mtandao, tunakuwa kama taa isiyo na umeme.

Tayari tumeshaifanya AI itutungie mashairi, itengeneze muziki na hata kutuchagulia vyakula na marafiki. Tunazidi kupoteza uhalisia wa maisha yetu. Mzee alikuwa akikueleza historia ya ukoo wako kutoka kizazi cha saba, na kila sentensi ilikuwa na maana. Leo, unaipa AI swali lile lile na baada ya sekunde mbili unapata jibu. Lakini halina roho, halina utamaduni, na mara nyingine halina usahihi.

Narudia: Huwezi kupiga tofali bila kuchanganya udongo. Wenetu wafundishwe kufanya kazi kabla ya kufundishwa matumizi ya akili mnemba. Tuepuke maendeleo ya kinyumenyume.