Wanandoa wauawa kikatili, miili yachomwa moto

Mbeya. Wanandoa wanaodaiwa kuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameuawa katika Kijiji cha Chafuma, wilayani Momba.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Jeshi la Polisi Agosti 23, 2025 tukio la mauaji lilitokea Kata ya Kapele iliyo Tarafa ya Ndalambo, juzi Agosti 22, saa nane mchana.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga imesema wanandoa hao waliuawa kikatili kwa kupigwa na kuchomwa moto na wananchi waliojichukulia sheria mkononi wakiwatuhumu kuhusika na mauaji ya Imbanji Simwaka (80), aliyekuwa mama mwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.

Amewataja waliouawa kuwa ni Babuloha mwenye umri kati ya miaka 26 na 28, pamoja na Jenifa Babuloha anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 23 na 25, ambao inaelezwa waliingia nchini kinyemela bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Kamanda Senga amesema Simwaka aliuawa usiku wa Agosti 19, 2025 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani.

Amesema mwili wake ulifukiwa bafuni nyumbani kwake na tangu Agosti 20, hakuonekana hali iliyozua wasiwasi miongoni mwa ndugu na wanakijiji.

“Kutokana na kutoonekana kwake ndipo wanakijiji walianza kumtafuta na ilipofika Agosti 22, 2025 waligundua kaburi la siri bafuni,” amesema katika taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Senga, wanakijiji walisambaza taarifa kuwa wanandoa waliopanga chumba nyumbani kwa Simwaka walikuwa wakiuza baadhi ya mazao yake, jambo lililoibua mashaka na hasira kwa jamii.

“Ndipo wananchi waliwakamata wanandoa hao na kuwakabidhi kwa uongozi wa kijiji kwa ajili ya taratibu za kisheria. Hata hivyo, kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa, kundi la wananchi lilivamia ofisi ya kijiji, kuvunja na kuwatoa washukiwa hao kwa nguvu, kisha kuwaua kwa kutumia silaha za jadi na kuchoma miili yao moto,” amesema.

Jeshi la Polisi limelaani matukio hayo mawili ya kikatili, pamoja na wananchi kujichukulia sheria mkononi ikieleza matendo hayo si tu ni kinyume cha sheria, bali pia yanahatarisha amani na usalama wa jamii.

“Uchunguzi wa kina unaendelea ili kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wote waliopanga, kushiriki au kuchochea tukio hili la mauaji,” amesema.

Kamanda Senga ametoa wito kwa wananchi mkoani Songwe kutokujichukulia sheria mkononi hata pale wanapokuwa na hasira au mashaka dhidi ya mtu au kikundi fulani, bali watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi wanapohisi au kushuhudia tukio la kihalifu.

Vilevile jeshi hilo limeonya tabia ya wananchi kuwapokea wageni wasiowafahamu, likielekeza kwamba watoe taarifa kwa viongozi wa kijiji ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Kamanda Senga amewataka kuheshimu taratibu za kisheria na kuelewa kuwa, haki haiwezi kupatikana kwa njia ya mabavu.