Dar es Salaam. Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), leo Jumamosi, Agosti 23, 2025 inakutana jijini Dodoma katika kikao cha kuteua wagombea wake wa ubunge na uwakilishi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kikao hicho kinachoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan kinahitimisha michakato mirefu iliyoanza Juni 28, 2025 kwa shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu. Kura za maoni na sasa ni uteuzi wa mwisho.
Watakaoteuliwa, watakuwa na kazi ya kupeperusha bendera ya CCM katika kampeni za uchaguzi huo kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28. Jumatano ya Oktoba 29, 2025 ndio siku ya upigaji kura kuchagua madiwani, wabunge na Rais.
Tayari Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefungua dirisha la kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hizo kuanzia Agosti 14 hadi Agosti 27 itakapofanya uteuzi.

Aidha, kikao hicho cha Halmashauri Kuu kinaweza kutoka na jina la Katibu Mkuu mpya wa CCM ambaye atavaa viatu vya Dk Emmanuel Nchimbi.

Hiyo ni kutokana na Dk Nchimbi kuwa mgombea mwenza mteule wa CCM katika uchaguzi mkuu. Kwa nafasi hiyo na pilikapilika za kampeni, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia anaweza kupendekeza jina la kada mwingine wa chama hicho kwa wajumbe wa kikao hicho ili kumteua.