Toldo ameibeba Madagascar mabegani | Mwanaspoti

KIPA mkongwe wa Madagascar, Ramandimbisoa Lalain’arijaka Michel ‘Toldo’, amekuwa sehemu ya mafanikio ya taifa hilo baada ya kufuzu hatua ya nusu fainali ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024.

Toldo, mwenye umri wa miaka 39 na anayekipiga klabu ya Elgeco Plus, mabingwa wa Ligi Kuu ya Madagascar na Kombe la Taifa nchini humo msimu uliopita, amecheza dakika zote za hatua ya makundi na robo fainali, akionyesha kiwango cha juu cha kuokoa michomo na kuipa Madagascar uhai katika kila mchezo.

Katika mechi nne za awali hatua ya makundi, Toldo ameokoa mashuti 15, akipata clean sheet mbili na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi mara tatu mfululizo.

Mchezo muhimu zaidi ulikuwa dhidi ya Mauritania ambapo Madagascar walimaliza wakiwa pungufu ya mchezaji mmoja, lakini kipa huyo aliokoa mashuti kadhaa na kuhakikisha matokeo yanabaki sare tasa.


Pia alifanya kama hivyo dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kabla ya kung’ara zaidi dhidi ya Burkina Faso kwa kuokoa mashuti saba na kusaidia ushindi wa mabao 2-1 uliowapeleka robo fainali.

Hadi timu hiyo inafuzu nusu fainali, ni Tanzania pekee iliyotikisa nyavu za kipa huyo mara mbili ambaye hadi sasa ameruhusu mabao manne kwenye nyavu zake. Kenya na Burkina Faso zimepata mojamoja.

Katika robo fainali dhidi ya Kenya, Toldo aliendelea kung’ara kwa kuokoa mashuti muhimu dakika za kawaida kabla ya kuwa shujaa kwenye mikwaju ya penalti akiokoa mmoja na mwingibe kutoka nje iliyoipeleka Madagascar nusu fainali kwa mara ya pili mfululizo.

Akizungumza na tovuti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Toldo alisema: “Ninajisikia kuheshimiwa sana. Kupata tuzo hii mara tatu si kwa bahati, bali ni matokeo ya kazi ngumu na jitihada za pamoja za timu.”

Madagascar si wageni katika mafanikio barani Afrika. Waliwahi kufika robo fainali ya AFCON mwaka 2019 na kushika nafasi ya tatu kwenye CHAN 2022. Hata hivyo, safari ya mwaka huu imekuwa ya kipekee kwani wao pekee ndiyo wawakilishi wa COSAFA waliobaki katika hatua ya nusu fainali.