McCarthy: Kesho yetu ni bora zaidi

IKISHIRIKI kwa mara ya kwanza michuano ya CHAN 2024, timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars imeishia hatua ya robo fainali huku kocha wa kikosi hicho, Benni McCarthy akisema anaona mambo mazuri zaidi siku zijazo.

Kenya iliyokuwa mwenyeji wa michuano hiyo kwa kushirikiana na Tanzania na Uganda, imepoteza mchezo wa robo fainali juzi Ijumaa kwa mikwaju ya penalti 3-4 kufuatia dakika 120 matokeo kuwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Madagascar.

Alphonce Omija, aliyefunga bao la Kenya kwa kichwa muda wa kawaida dakika ya 48 na kuiweka mbele timu yake kabla ya Madagascar kusawazisha dakika ya 69, ndiye aliyekosa penalti ya mwisho iliyowaondosha wenyeji hao. Kabla ya hapo, mtangulizi wake Michael Kibwage naye alikosa penalti.

McCarthy, ambaye amewapeleka Harambee Stars robo fainali katika ushiriki wao wa kwanza kabisa kwenye mashindano hayo, alisema morali na mapambano ya wachezaji wake vinastahili pongezi kuliko huzuni ya kutolewa.

“Ni fahari tupu kwa kile tulichokifanya. Wachezaji walijituma kila siku mazoezini na kwenye mechi zote. Lakini mpira ndivyo ulivyo, penalti wakati mwingine ni bahati tu,” alisema McCarthy na kuongeza.

“Ilikuwa ngumu kutolewa kwa njia hii. Tulitarajia mchezo mgumu lakini si kwa kiwango walichoonyesha. Naipongeza Madagascar kwa kufuzu nusu fainali. Ukiweza kucheza kwa ujasiri mbele ya mashabiki wenye shauku na kelele nyingi kama hizi, unastahili pongezi kubwa.”

Kocha huyo alikiri timu yake ingeweza kufunga mapema na kufanikisha ushindi kama wangetumia vizuri nafasi walizopata.

“Ilipaswa kuwa mchezo wa upande wowote. Tumekosa nafasi muhimu na hatimaye tumepoteza. Ukikosa kutumia nafasi zako, mpira huwaadhibu,” alifafanua.

Kenya licha ya kufunga bao kila mechi kwenye mashindano hayo, lakini tatizo kubwa lilionekana kushindwa kufunga zaidi ya bao moja kwa mchezo, jambo ambapo linatajwa kuigharimu dhidi ya Madagascar.

Timu hiyo iliibuka kinara wa kundi A lililokuwa na miamba kama Morocco, Zambia na DR Congo, huku ikiruhusu mabao mawili pekee katika mechi tano ilizocheza hadi inatolewa.

McCarthy anaamini mafanikio hayo ni msingi wa mustakabali bora wa timu ya taifa ya Kenya ambapo alisema: “Leo tuna huzuni, lakini tukitazama nyuma tulivyoweza kushinda kundi gumu zaidi, hatuna budi kujivunia.

“Tunajisikia vibaya sasa, lakini kesho nikikaa chini kutafakari, nitajivunia tulichokifanya. Tunapaswa kuendelea kujenga misingi mizuri ili timu ya taifa iwe imara zaidi ya hivi ilivyokuwa.”