Gwalala kutimkia Mbeya City | Mwanaspoti

KIUNGO wa zamani wa Coastal Union, Greyson Gwalala yupo katika hatua ya mwisho kumalizana na Mbeya City iliyopanda daraja kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao 2025-2026.

Gwalala anaungana na Ame Ally aliyetua Mbeya City akitokea Mashujaa, Yahya Mbegu (Singida Black Stars), Habib Kyombo aliyekuwa akiitumikia Pamba Jiji kwa mkopo akitokea Singida Black Stars kama ilivyokuwa kwa Beno Kakolanya aliyekuwa Namungo.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa mchezaji huyo kimelithibitishia Mwanaspoti kuwa tayari kiungo huyo amefikia makubaliano na timu hiyo, hivyo muda wowote anaweza kusaini mkataba.

“Ni kweli alikuwa na mazungumzo na timu hiyo na kufikia makubaliano, hivyo muda wowote anaweza akasaini mkataba wa kuitumikia Mbeya City ambayo imeahidi kurejesha ushindani katika ligi,” alisema.

“Haikuwa rahisi kumshawishi kiungo huyo ambaye mbali na City alikuwa na ofa nyingine kutoka timu zinazoshiriki ligi kuu, lakini kutokana na mipango mikakati ya timu hiyo ameona ni timu sahihi kwake.”

Mwanaspoti lilimtafuta kiungo huyo kufahamu ukweli wa taarifa hizo ambapo alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sasa lakini msimu ujao atacheza ligi kuu.

“Nimemaliza mkataba na Coastal Union lakini tayari nimefanya mazungumzo na moja ya timu ambayo siwezi kuweka wazi kwa sababu bado hatujamalizana, lakini naamini mambo yakiwa sawa kila kitu kitawekwa wazi uhakika ni kwamba nitacheza ligi kuu msimu ujao.”