Asilimia 78 ya kaya nchini zina uhakika wa vyoo salama

Hanang. Kaya zenye vyoo bora nchini zimefikia asilimia 78 huku asilimia 1.2 zikiwa hazina vyoo huku katika Mkoa wa Manyara, asilimia 6.4 ya kaya zake hazina vyoo salama.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 23, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), anayeshughulikia sekta ya afya, Profesa Tumaini Nagu katika hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Ibrahim Mbogo.

Mbogo amesoma hotuba hiyo kwenye uzinduzi wa mradi wa kuboresha upatikanaji wa huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira zenye kuzingatia utu na mazingira salama ya kujifunza katika shule ya msingi Bashang iliyopo katika Kata ya Wareta, wilayani Hanang.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Ibrahim Mbogo (katikati) akikagua mradi wa kuboresha upatikanaji wa huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira katika shule ya msingi Bashang wilayani Hanang’. Picha na Joseph Lyimo



Kwa mujibu wa sense ya watu na makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina kaya binafsi 14,152,803. Kati ya hizo, kaya 13,776,975 (sawa na asilimia 97.3) zipo Tanzania Bara na kaya 378,828 (asilimia 2.7) zipo Zanzibar.

Mbogo amesema karibu asilimia 36 ya kaya katika halmashauri ya Wilaya ya Hanang wanatumia vyoo ambavyo siyo bora kwa maana kwamba havikidhi mahitaji ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza.

“Hali hii inahitaji serikali katika ngazi ya mkoa na halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kila inakuwa na choo bora,” amesema Profesa Nagu.

Amesema katika kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira, Serikali imejenga miundombinu ya maji, vyoo bora na eneo la unawaji katika shule 2,264 katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Amesema Serikali kupitia mradi endelevu wa huduma za maji na usafi vijijini (SRWSSP) imekuwa ikihakikisha suala la upatikanaji wa huduma za maji, vyoo bora na sehemu ya unawaji mikono (wash).

“Nawapongeza sana shirika la Water Aid Tanzania kwa kuunga juhudi hizi za Serikali kwa kujenga miundombinu ya maji, vyoo bora na ile ya kunawa mikono katika shule hii ya msingi Bashang.

“Huu ni uthibitisho tosha wa ufanyaji kazi unaozingatia vipaumbele vya Serikali katika kuwahudumia Watanzania na hususani wanafunzi na walimu wetu katika shule hii,” amesema Profesa Nagu katika hotuba hiyo iliyosomwa na Mbogo.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Ibrahim Mbogo (katikati) akikagua mradi wa kuboresha upatikanaji wa huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira katika shule ya msingi Bashang wilayani Hanang’. Picha na Joseph Lyimo



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga amesema wataendelea kusaidia eneo la Hanang, ndiyo sababu wamejenga vyoo vya wanafunzi na walimu wa shule ya msingi Bashang.

Mzinga amesema wamewezesha upatikanaji wa huduma za maji na usafi na kuweka mikakati ya ubunifu na usanifu miradi ya ‘Wash’.

Mratibu wa shirika la Water Aid Tanzania Wilaya ya Hanang, Upendo Mtambo amesema mpango wao ni kuwezesha Hanang kuwa eneo la kijiografia katika kuteketeza miradi ya Wash.

Naye mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo, Mathias Ombay amesema wamepokea miundombinu hiyo ya matundu 23 vya vyoo na kuahidi kushirikiana na wenzake kuvitunza.

Amesema wanafunzi 796 wa shule hiyo wamefurahi kujengewa vyoo vipya kwani vile vya awali miundombinu yake siyo mizuri.

Mkazi wa Kijiji cha Bashang, Magdalena Lowri amesema wanashukuru kwa miundombinu mipya ya vyoo vya shule hiyo kujengwa.