Tanzania yaanzisha kitengo cha uchunguzi wa moyo cha kimataifa

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imeanzisha kitengo cha uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo wa Afrika Mashariki na Kati, ili kutambua afya zao kabla ya kushiriki mashindano mbalimbali.

Hatua hio inaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili barani Afrika baada ya Misri kuanzisha kitengo maalumu cha uchunguzi wa moyo kwa wanamichezo.

Kitengo hicho kitaangazia upimaji wa afya ya moyo, uhamasishaji kuhusu magonjwa ya moyo, pamoja na kufanya tafiti kwa lengo la kuzuia vifo vya ghafla vinavyotokana na matatizo ya moyo kwa wanamichezo.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI, ambayo yaliambatana na utiaji  saini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Chama cha Moyo cha Afrika na Misri (EAHA), Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, ameeleza umuhimu wa haraka wa huduma hizo.


“Tanzania imebarikiwa kuwa na wanamichezo wenye vipaji pamoja na vilabu vya michezo vilivyo hai, lakini nyuma ya shangwe na nishati hiyo kuna ukweli usiofahamika sana, hata wanamichezo walioko katika kilele cha uimara wa mwili hawawezi kuepuka matatizo ya moyo.

“Tunatoa wito kwa wanamichezo wote kufanyiwa uchunguzi kabla ya kushiriki michezo yoyote. Kimataifa, tumeshuhudia visa vya vifo vya ghafla vinavyotokana na mshtuko wa moyo wakati wa mazoezi au mashindano, mara nyingi kwa vijana wanaoonekana kuwa na afya njema. Matukio haya ya kusikitisha yanaweza kuzuilika kwa uchunguzi sahihi, ufuatiliaji na matibabu kwa wakati,” amesema Dk Kisenge.

Mratibu wa Kitengo cha Moyo kwa Wanamichezo, Dk Eva Wakuganda, amesema wanamichezo 150 tayari wamefanyiwa uchunguzi.


Amesema JKCI imeanza kushirikiana na vilabu vikubwa kama Simba na Yanga, pamoja na shule mbalimbali, ili kushiriki katika mpango huo.

“Tanzania ina zaidi ya watu milioni 10 wanaoshiriki michezo. Kadri mtu anavyojifua zaidi, ndivyo mabadiliko yanavyotokea katika mfumo wa upumuaji, misuli na moyo. Uchunguzi wa afya ya moyo ni muhimu kwani vifo vya ghafla vimeripotiwa hata katika nchi zilizo na vitengo vya juu vya moyo kwa wanamichezo,” amesema.

Dk Eva ameongeza kuwa mradi huo haujalenga tu kuongeza uelewa, bali pia kuwafikia wanamichezo kote Tanzania, Afrika Mashariki na Kati.

“Tunatarajia kupima wanamichezo, kuwapa elimu kuhusu vifo vya ghafla vinavyotokana na matatizo ya moyo, kutoa vifaa vya kuokoa maisha na kuchangia tafiti kubwa barani Afrika,” amesema.

Kwa upande wa ushirikiano wa kikanda, Profesa Amned Eissa, mshauri wa masuala ya tiba ya moyo ya kimataifa na ya michezo kutoka EAHA, alisema makubaliano hayo yatasaidia kubadilishana maarifa hasa kwenye masuala ya magonjwa ya moyo kupitia michezo.

“Ushirikiano utaanza kwa kutoa mafunzo ya ana kwa ana kwa madaktari wa Kitanzania kuhusu namna ya kufanya uchunguzi kwa wanamichezo. Katika miezi ijayo, kundi la madaktari kutoka Tanzania litakwenda Misri kwa ajili ya kupata uzoefu wa moja kwa moja,” amesema Eissa.