Morogoro. Wahitimu wa mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba (mgambo) katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wameiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma kwa kuwapatia ajira ndani na nje ya wilaya hiyo ili kujikimu kimaisha na kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama.
Wahitimu hao wametoa ombi hilo leo kwenye hafla ya kufunga mafunzo hayo ya awali ya Jeshi la Akiba, kikundi cha 47/2025, yaliyofanyika katika Tarafa ya Mngeta iliyopo katika Halmashauri ya Mlimba.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Flora Keneth amesema uzoefu unaonyesha askari wa jeshi hilo wanapomaliza mafunzo huishia kuachwa na kulandalanda mtaani bila ajira za kudumu kwenye taasisi, kampuni na maeneo mengine ambayo wanaweza kuajiriwa.
“Mkuu wa Wilaya, leo tumehitimu mafunzo yetu, tupo timamu kiakili na kimwili, ikikupendeza tunaomba mtutumie katika shughuli mbalimbali za kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama, msituache tukabaki mtaani tukilandalanda,” amesema Flora.
Akijibu kilio chao, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mlimba, Jamary Abdul, kuhakikisha anawapatia vijana hao kazi za ulinzi katika maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo yenye miradi ya Serikali zikiwemo shule, zahanati na masoko.
Aidha, amemuagiza Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kilombero (OCD) kuhakikisha anafanya ukaguzi kwenye kampuni zote za ulinzi wilayani humo na kuchukua hatua ya kuwaondoa askari wote wasiopitia mafunzo ya Jeshi la Akiba.
“Nimepita sehemu moja nimekuta kuna mzee wa miaka 80 analinda wakati hata kufungua mlango hawezi na hajapitia mafunzo ya Jeshi la Akiba, hiyo haiwezekani kwa kuwa hatufanyi kazi kwa upendeleo au huruma, kampuni zote za ulinzi zinazoajiri walinzi wasiopitia mafunzo zifuatiliwe,” amesema Kyobya.
Kyobya katika kuhakikisha vijana wahitimu wa Jeshi la Akiba wanapata ajira, ameziagiza mamlaka za uhifadhi ambazo ni TFS na Tawa kuhakikisha wanawatumia vijana hao kama walinzi wasaidizi katika kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yote ya uhifadhi.
Kwa upande wake, Mshauri wa Mgambo katika Wilaya ya Kilombero, Luteni Kanali Ulrick Munisi ameeleza kuwa elimu waliyoipata askari hao katika mafunzo hayo ni pamoja na kwata, mbinu za kivita, mbinu za medani, kulenga shabaha, sheria za jeshi na muundo wa Jeshi la Akiba, Polisi Jamii na ukakamavu.
Ametaja elimu nyingine kuwa ni pamoja na urai, mafunzo ya zimamoto, uhifadhi, kupambana na kuzuia rushwa, nidhamu na ujasiri, utii na uaminifu ambapo masomo hayo yote yatawasaidia katika kutekeleza majukumu yao sehemu mbalimbali watakazofanyia kazi.