MWANAISHA MNDEME AJITOSA RASMI KUGOMBEA UBUNGE KIGAMBONI KUPITIA ACT-WAZALENDO


Wakili na mwanaharakati wa haki za kijamii, Mwanaisha Mndeme, leo ameonesha dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Kigamboni kwa kuchukua fomu ya kugombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

Zoezi hilo limefanyika katika ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na kushuhudiwa na wafuasi wake waliokusanyika kwa hamasa kubwa kuonyesha mshikamano na matumaini ya mabadiliko.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Mndeme amesema:

“Dhamira yangu ni kuhakikisha Kigamboni inapata mwakilishi wa kweli anayesikiliza na kuwasemea wananchi bungeni. Tutapigania miundombinu bora ya barabara, huduma nafuu na za uhakika za vivuko, na kupunguza gharama ya matumizi ya Daraja la Mwalimu Nyerere.”

Ameeleza kuwa, licha ya matarajio kuwa daraja hilo lingekuwa mkombozi wa usafiri, limegeuka kuwa mzigo kwa wakazi wa Kigamboni. Kwa mujibu wake, ACT-Wazalendo imejipanga kuleta mabadiliko yenye tija na kuifanya Kigamboni kuwa mfano wa maendeleo jumuishi.

“Naamini Kigamboni inaweza kuwa mfano wa maendeleo yanayomjali mwananchi. Pamoja, tunaweza,” amesema kwa msisitizo.

Hatua ya Mwanaisha Mndeme kuingia rasmi katika kinyang’anyiro cha ubunge inazidi kuashiria ushindani mkali unaotarajiwa katika uchaguzi mkuu ujao, huku ajenda ya maendeleo kwa wananchi ikiwekwa mbele na vyama mbalimbali.