Dar es Salaam. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiteua wagombea ubunge na uwakilishi watakaopeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, pia kimemteua Dk Asha-Rose Migiro kuwa katibu mkuu wake mpya.
Uteuzi huo umetangazwa leo Agosti 23, 2025 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, makao makuu ya CCM, jijini Dodoma ikiwa ni mara yake ya mwisho, kwa kuwa nafasi hiyo sasa itakuwa chini ya Kenani Kihongosi.
Majina hayo yamewekwa hadharani baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kilichoketi leo Agosti 23 na kufanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wanachama walioomba nafasi za ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa majimbo na viti maalumu.
Makalla mbele ya vyombo vya habari amesema huo ndiyo mwisho wa mchakato.
“Hili ndiyo hitimisho, kwamba CCM imepata wagombea watakaokwenda kupeperusha bendera kuinadi ilani ya CCM katika uchaguzi mkuu,” amesema akiwashukuru waandishi wa habari kwa ushirikiano waliompa akiwa mwenezi na kuwaomba kumpa ushirikiano huohuo Kihongosi.
Katika orodha ya walioteuliwa iliyotangazwa na Makalla, baadhi ya wanasiasa mashuhuri wameachwa licha ya kuongoza katika kura za maoni za CCM zilizopigwa Agosti 4, 2025.
Aliyekuwa mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu ni miongoni mwa walioachwa katika uteuzi.
Wengine waliowekwa kando ni Fredrick Lowassa wa Monduli, ambaye ni mtoto wa hayati Edward Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu.
Wamo pia Constantine Kanyasu wa Geita Mjini na Stanislaus Mabula wa Nyamagana.
Katika uteuzi huo, waliokuwa miongoni mwa wabunge 19 wa Chadema waliohamia CCM na kujitosa kwenye mbio za ubunge wameteuliwa kushiriki kinyang’anyiro hicho.
Walioteuliwa na majimbo yao kwenye mabano ni Kunti Majala (Chemba), Esther Matiko (Tarime Mjini), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Jesca Kishoa (Iramba Mashariki) na Hawa Mwaifunga (Tabora Mjini).
Katika kura za maoni ndani ya chama hicho, Kishoa na Kunti ndio walioongoza. Bulaya, Mwaifunga na Matiko walishika nafasi ya pili, ya tatu na ya nne.
Katika jimbo la Kigoma Mjini, msanii wa muziki, Clayton Chipando maarufu Baba Levo amepitishwa kuwania ubunge kupitia CCM, akiachwa Kirumbe Ng’enda aliyerongoza kura za maoni. Baba levo amewahi kuwa diwani wa Mwanga Kaskazini kupitia ACT-Wazalendo.
NEC ya CCM imemthibitisha Dk Asha-Rose Migiro kuwa Katibu Mkuu wake, akiwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1977.
Dk Migiro anakuwa katibu mkuu wa 13 baada ya makatibu wakuu wengine, Pius Msekwa (1977-1981), Balozi Daudi Mwakawago (1981-1984), Rashid Kawawa (1982-1990), Horace Kolimba (1990-1995), Dk Lawrence Gama (1995-1997), Philip Mangula (1997-2007), Yusuf Makamba (2007-2011).
Wengine ni Wilson Mukama (2011-2012), Abdulrahman Kinana (2012-2018), Dk Bashiru Ally (2018-2021), Daniel Chongolo (2021-2023) na Dk Emmanuel Nchimbi (2024-2025).
Kuthibitishwa kwa Dk Migiro kunamfanya kuweka historia katika wadhifa huo wa utendaji ndani ya CCM, huku Mwenyekiti wa chama hicho Taifa akiwa pia mwanamke, Rais Samia Suluhu Hassan.
NEC pia imemthibitisha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Makalla, ambaye Rais Samia amemteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Vilevile imemteua Joshua Mirumbe kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha, nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Dk Frank Haule, aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe.
NEC pia imemteua Halid Mwinyi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuchukua nafasi ya Jokate Mwengelo.
Dk Asha-Rose Mtengeti Migiro (alizaliwa Julai 9, 1956) ni mwanasiasa na mwanadiplomasia aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuanzia mwaka 2007 hadi 2012.
Aliteuliwa kuwa Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimwi barani Afrika Julai 13, 2012.
Dk Migiro aliingia kwenye siasa na kugombea ubunge wa viti maalumu kupitia CCM kwa upande wa taasisi za elimu ya juu. Pia, aliwahi kuwa Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM.
Kabla ya hapo aliwahi kuwa mjumbe wa kata kupitia CCM kutoka 1994 hadi 2000, na mjumbe wa Baraza la Utekelezaji la Mkoa kutoka 2000 hadi 2005. Kuanzia mwaka 2000 hadi 2006, alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Januari 4, 2006, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa baada ya aliyekuwa waziri, Jakaya Kikwete, kuchaguliwa kuwa Rais na kuunda baraza jipya la mawaziri. Alikuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo tangu Tanzania ipate uhuru.
Migiro aliteuliwa kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Ban Ki-moon, Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa kutoka Korea Kusini, Januari 5, 2007. Kwa mujibu wa Ban, “Yeye ni kiongozi anayeheshimika sana ambaye amekuwa mtetezi wa masilahi ya nchi zinazoendelea kwa miaka mingi.”
Wakati wa utumishi wake katika Umoja wa Mataifa, Dk Migiro pia alikuwa mjumbe wa Tume ya Ushirikiano wa Maendeleo Ufanisi na Afrika iliyoundwa na Waziri Mkuu wa Denmark, Anders Fogh Rasmussen, na iliyofanya mikutano kati ya Aprili na Oktoba 2008. Migiro alihudumu kama Naibu Katibu Mkuu hadi Juni 2012.
Baada ya kumaliza utumishi wake katika Umoja wa Mataifa, Dk Migiro alirudi Tanzania na kuteuliwa kuwa waziri katika baraza la mawaziri la Rais Jakaya Kikwete.
Aligombea kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia CCM katika uchaguzi wa mwaka 2015, lakini hakufanikiwa kupata uteuzi, Dk John Magufuli alishinda.
Rais Magufuli alimteua Dk Migiro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mei 2016.
Kihongosi amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa, amekuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa Jumuiya ya Vyuo Vikuu Tanzania (Tahliso), amekuwa mjumbe wa Kamati ya Siasa Tawi, mjumbe wa Kamati ya siasa kata, mjumbe halmasahuri kuu ya wilaya, mjumbe wa Kamati ya siasa ya mkoa.
Pia, amewahi kuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya mkoa, mjumbe wa Baraza kuu UVCCM Taifa, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, amewahi kuwa mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa.
Kihongosi amewahi kuwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, amekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha na baadaye alihamishiwa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida na amewahi kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa.