KUNA mambo flani yanasonga pale Msimbazi yalipo makao makuu ya Klabu ya Simba, ambapo vigogo wanapambana kuweka mambo sawa, kwani kuna mastaa ambao zipo kila dalili kwamba wanapaswa kusepa huku wengine ambao hawajaripoti wakitakiwa kutua kikosini.
Kumbuka wanaotakiwa kusepa ni baadhi ya wale wa zamani na lengo ni ili kupisha sura mpya ambazo zimeshanaswa. Lakini wakati unasoma hapa wanaopaswa kupisha wangalipo kikosini.
Unaambiwa Mnyama bado yupo zake Misri akiendelea kujiweka imara huku ikielezwa kuwa benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids lina takriban siku nne hadi tano za moto ili kujiimarisha kabisa.
Kikosi hicho kiliondoka Dar es Salaam Julai 30 mwaka huu na kupiga kambi Jiji la Ismailia pale Misri ambapo ilikaa kwa takribani wiki mbili na kucheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Kahraba Ismailia kabla ya Agosti 15 kuelekea Cairo hukohuko Misri ilipocheza mechi mbili dhidi ya ENPPI na Al Zulfi.
Hadi kufikia leo Agosti 24, Simba itakuwa imefikisha siku 23 ikiwa huko Misri na kubakiwa na siku saba kabla ya kurudi, lakini nne hadi tano kati ya hizo ndizo zitakuwa za moto.
Kiongozi mmoja wa Simba aliyepo kambini nchini Misri, ameliambia Mwanaspoti kwamba, mwisho wa mwezi huu wanatarajia kurudi Dar kuendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Mtoa taarifa huyo aliendelea kubainisha kwamba, katika kipindi hiki kilichobaki kabla ya kurudi Dar, benchi la ufundi lipo katika hatua za mwisho kukamilisha mikakati iliyoianza ya kuijenga timu.
“Wiki hizi za mwisho za kumalizia maandalizi ya kabla ya kuanza kwa msimu ndiyo kunakuwa na zile program za kiufundi zaidi, hivyo muda uliobaki benchi la ufundi linautumia vizuri,” alisema mtu huyo.
Katika hatua nyingine, wachezaji watano wa Simba waliokuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kikishiriki michuano ya CHAN 2024 na kuondoshwa hatua ya makundi, Shomari Kapombe, Yusuph Kagoma, Abdulrazack Hamza, Yakoub Suleiman na Wilson Nangu, hawataenda Misri na badala yake wataisubiri timu hiyo irudi Dar ili kuungana na wenzao.
Chanzo kutoka Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa, baada ya Stars kuondoshwa kwenye michuano ya CHAN 2024, imewapa mapumziko wachezaji wake waliokuwa na kikosi hicho.
“Wale wachezaji waliokuwa na kikosi cha Stars watabaki hukohuko Dar, wataisubiri timu irudi ili kuungana na wenzao kuendelea na maandalizi yaliyobaki.
“Kitendo cha kuwaambia waje huku Misri ni kama kuwachosha kwani siku zimebaki chache na wao walikuwa kwenye majukumu ya kulitumikia taifa, tunaamini mazoezi waliyokuwa wakiyafanya wakiwa na Stars yameendelea kuwaweka fiti,” alisema bosi huyo.
Hadi sasa, Simba imetambulisha wachezaji wapya tisa ambao ni Anthony Mligo, Naby Camara, Rushne De Reuck, Alassane Kante, Semfuko Charles, Morris Abraham, Mohammed Bajaber, Neo Maema na Jonathan Sowah, huku kipa Yakoub Suleiman na beki Wilson Nangu wote kutoka JKT Tanzania ikielezwa imemalizana nao ikisubiri kuwatangaza rasmi ambapo jumla yake itakuwa 11.
Yakoub na Nangu walikuwa kwenye kikosi cha Stars kilichoshiriki michuano ya CHAN 2024 ambapo wanaungana na Kapombe, Kagoma na Hamza kuendelea kubaki Dar wakisubiri wenzao warudi.
Katika muda huo uliobaki, taarifa kutoka kambi ya Simba huko Misri zinasema itategemea na uamuzi wa kocha kama anahitaji mchezo mwingine wa kirafiki kabla ya kurudi Dar watacheza.
“Tumecheza mechi kadhaa za kirafiki tukiwa hapa, lakini siwezi kusema moja kwa moja kwamba ndiyo basi, bali kocha akiona inafaa timu inaweza kucheza kisha tutarudi nyumbani kumalizika maandalizi yaliyobaki kabla ya kuanza kwa msimu mpya,” kilisema chanzo hicho.
Hadi kufikia sasa, Simba imecheza mechi tatu za kirafiki ikiwa huko Misri ikianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kahraba Ismailia, kisha ikapoteza 4-3 mbele ya ENPPI na kuichapa Al Zulfi ya Saudi Arabia bao 1-0.