KWA muda mrefu timu kongwe za Yanga na Simba zilikuwa zikipigana vikumbo katika kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji kutoka DR Congo ambaye hivi karibuni ametoka kuiwakilisha nchi yake kwenye michuano ya CHAN 2024 inayoendelea Tanzania, Kenya na Uganda.
Licha ya timu hizo kongwe zenye maskani katika mitaa ya Jangwani na Msimbazi iliyopo Kariaako, Dar es Salaam, kufanya mazungumzo mara kadhaa na mabosi wa timu inayommiliki mchezaji huyo, lakini zote zimeshindwa kufanikisha dili hilo katika mazingira ambayo yameacha sintofahamu nyuma yake.
Nyota huyo, Agee Basiala Amongo, aliyekuwa akikipiga AS Maniema ya DR Congo ambapo sasa rasmi amezitosa ofa za Yanga na Simba baada ya kusaini mkataba wa kuichezea FC Saint Eloi Lupopo ya hukohuko kwao – DR Congo.
Lupopo imemtambulisha mchezaji huyo ikisema: “Jina la kukumbukwa, mchezaji wa kuigwa: Agee Basiala sasa ni wetu!
Historia inaandikwa mbele ya macho yetu. Jiandae kushuhudia hatua ya kihistoria. Klabu ya St Eloi Lupopo inajivunia kumkaribisha Agee Basiala, kipaji cha kipekee, msanii wa dimbani, mchezaji anayejumuisha ari na ubora wa hali ya juu. Ujio wake kwa mkataba wa misimu miwili unaashiria enzi mpya kwa klabu yetu.
“Agee Basiala Amongo alianza kung’ara akiwa na klabu yake ya zamani, AS Maniema Union, katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pia akiitumikia timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika hatua ya makundi ya CHAN 2024. Kipaji chake kikubwa kimevuka mipaka ya Congo, kikivutia macho ya klabu kubwa barani Afrika na duniani. Heshima hii kutoka kwa majina makubwa ya soka inathibitisha upeo wa uwezo wake na athari alizoacha uwanjani.
“Klabu inayopendwa na Rais Jacques Kyabula, licha ya ushindani mkali katika harakati za usajili huu, imefanikiwa kwa fahari kubwa kumsajili Agee Basiala, ambaye alivutiwa na mradi wetu na kuamua kujiunga nasi.”
Ikumbukwe kuwa, nyota huyo alianza kuhusishwa na Yanga kwa muda mrefu kutokana na ukaribu wa mabosi wa kikosi hicho na AS Maniema Union, kisha baada ya hapo Simba ikajitosa pia kuingilia dili hilo, ingawa imeshindikana na mwenyewe kuamua kubakia kwao Congo.
Mbali na Yanga na Simba zilizoonyesha nia ya kumuhitaji, matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC msimu huu ilionyesha pia nia ya kumsajili na hasa baada ya ujio wa kocha mkongomani mwenzake, Florent Ibenge anayemjua vizuri uchezaji wake.
Basiala aliyezaliwa Desemba 29, 1998, ni miongoni mwa nyota wenye kipaji kikubwa kiasi cha kuzivutia timu mbalimbali za kwao DR Congo na hata Tanzania, ambapo kiu ya mashabiki wengi nchini ilikuwa kumuona akicheza moja ya klabu hizo kubwa.
Nyota huyo aliingoza DR Congo katika Michuano ya CHAN 2024 na kumaliza nafasi ya tatu kundi A na pointi sita, nyuma ya Morocco iliyomaliza nafasi ya pili na pointi tisa, huku wenyeji Kenya iliyotolewa robo fainali ikiongoza na pointi 10.
Katika michuano hiyo ya CHAN 2024 inayoendelea kuchezwa kwenye nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, Basiala alitoa asisti mawili akiwa na kikosi hicho cha DR Congo, huku akionyesha soka safi licha ya kutolewa hatua ya makundi.
Yanga iliwahi kumtaka Basiala msimu mmoja uliopita ikivutiwa naye wakati huo akicheza kama kiungo wa pembeni, lakini baadaye akabadilishiwa nafasi na kuchezeshwa kiungo wa kati mshambuliaji nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.
Timu hiyo ilirudi tena wakati wa dirisha dogo la Desemba – Januari, mwaka huu ambapo makubaliano yalifanyika yakilenga kufanikisha dili lake baada ya msimu kumalizika na kwamba, kila kitu kilitarajiwa kuwa hadhari katika dirisha hili la usajili linaloendelea.
Ndani ya Maniema ndiko alikotoka Maxi Nzengeli na wakati akiwa hapo, Basiala alichukuliwa kama pacha wake – wote wakiifanya timu hiyo kuwa tishio kabla ya Yanga kumnyakua fundi huyo na baadaye ilitaka kumnasa pacha wake lakini haikuwa hivyo. Mwanaspoti linafahamu kwamba mabosi wa Yanga na Maniema wana ukaribu mkubwa, hivyo klabu hizo zimekuwa zikifanya biashara nzuri ya wachezaji bila ya vikwazo vingi. Yanga katika kuimarisha eneo lao la kiungo mshambuliaji, imewasajili Offen Chikola, Lassine Kouma, Mohamed Doumbia na Celestin Ecua.
Juni 2025, Mwanaspoti liliripoti kwamba mabosi wa Simba kazi ilibaki kuwa kwao tu kwani walitakiwa ‘kuvunja’ benki ili kuinasa saini ya Basiala baada ya klabu AS Maniema kuweka hadharani dau la kumuuza nyota huyo.
Basiala alikuwa akiwindwa na Simba akitajwa kama mbadala sahihi iwapo Jean Charles Ahoua angetimkia Afrika Kusini alikokuwa akiwindwa na Kaizer Chiefs inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi.
Taarifa za ndani zililidokeza Mwanaspoti kwamba, mabosi wa Maniema walikuwa wakizungumza na wenzao wa Msimbazi na tayari waliwekewa mezani dau la kumbeba.
“Simba ilipewa rasmi dau la kumpata kiungo huyo, huku ikitakiwa kumnunua kwa Dola 150, 000 (zaidi ya Sh390 milioni),” kilisema chanzo hicho. Hata hivyo, Simba haikufanikisha dili hilo hadi mchezaji huyo kuibukia Lupopo, huku yenyewe ikimbeba Neo Maema ambaye tayari imemsajili na kumtambulisha baada ya kuachana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Mwingine ambaye Simba imemsajili katika eneo hilo la kiungo mshambuliaji ni Mohammed Bajaber aliyetokea Kenya Police.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Maniema, Guy Kapya alinukuliwa akisema: “Tulikuwa na mazungumzo na kiongozi mmoja wa Simba alileta ofa yao akimtaka Agee, lakini bado tulikuwa tunapambana nao, hawakufika tunapotaka.”
Julai 2025, pia Mwanaspoti liliripoti juu ya Basiala kutakiwa na Azam ikiwa ni siku chache baada ya klabu hiyo kumshusha kocha mwenye wasifu mkubwa barani Afrika, Florent Ibenge.
Ilielezwa kwamba, Azam iliamua kutumia turufu ya kuwa na Ibenge, ili kumlainisha nyota huyo kutua kwa matajiri hao kwa kuweka mkwanja wa maana.
Taarifa zilibainisha kuwa, Azam ilitua rasmi Maniema ikimtaka kiungo huyo pamoja na mshambuliaji matata Jephte Kitambala ambaye tayari imefanikiwa kuinasa saini yake.
Ibenge ndiye aliyependekeza usajili wa kiungo huyo anayeweza kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji sambamba na Kitambala ambaye ndiye imefanikiwa kumnasa.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa soka la DR Congo, Basiala mwenye uwezo wa kucheza kama winga na kiungo mshambuliaji, ana nguvu ya kumudu kukimbia eneo kubwa uwanjani kama alivyo Nzengeli na pia anajua kutoa pasi za mwisho na kuchezesha timu, lakini pia ni fundi wa kutupia mipira ya adhabu kama Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga kabla ya hivi karibuni kuuzwa Wydad Casablanca ya Morocco.