Hiki hapa chanzo valvu za moyo kuharibika

Dar es Salaam. Wazazi wamehimizwa kuwatibu watoto wanaopata ugonjwa wa mafindofindo (tonsillitis) mapema na kwa wakati ili kuwaepusha na hatari ya kupata magonjwa ya valvu za moyo.

Hayo yamesemwa na Daktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Salehe Mwinchete wakati wa kambi  ya siku nne ya upasuaji wa moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani.

Katika takwimu za JKCI magonjwa ya valvu za moyo kwa wagonjwa wa marudio mwaka 2021 ilikuwa ni asilimia 3.9, katika kundi la watu wa umri mdogo chiniya miaka 45 ulikuwa wa pili kwa ukubwa, ukipatikana kwa asilimia 8 ya wagonjwa wa umri huo.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 JKCI ilitoa huduma ya kubadilisha valvu za moyo kwa wagonjwa zaidi ya 100, huku takwimu zikionyesha ongezeko la wanaifanyiwa upasuaji wa valvu za moyo kuongezeka kati ya mwaka 2017 hadi 2024.

Dk Salehe amesema tatizo la valvu za moyo kuziba huanza na maambukizi ya kooni yajulikanayo kama mafindofindo (tonslight), na homa za utotoni za mara kwa mara ambazo huleta maambukizi yanayoathiri koo na wadudu wake kwenda kuharibu milango ya moyo (Valvu za moyo).

Ameongeza kuwa wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapougua mafindofindo ni muhimu wakamuona daktari ili waweze kutibiwa na dawa za antibiotics kwa usahihi, kusaidia kuzuia uharibifu katika milango ya moyo.

“Katika kambi hii iliyomalizika jana (juzi) tumewafanyia uchunguzi wagonjwa 30 ambapo kati yao 10 tumewafanyia upasuaji wa kuzibua valvu za moyo kwa kupitia tundu dogo”, amesema Dk Salehe

Dk Salehe amesema wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa tundu dogo katika kambi hiyo wana magonjwa ya valvu za moyo ambapo mlango mmoja katika upande wa kushoto wa moyo unakuwa umeziba au unavujisha damu.

“Dalili za awali za ugonjwa huu ni pamoja na kukosa pumzi, kuchoka, moyo kwenda mbio, kuzimia mara kwa mara, watu wanapopata dalili hizi wafike katika Taasisi yetu kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa moyo kwani itawasaidia kugundua tatizo mapema na kuwaepusha kufikia hatua ya kwenda kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua”, amesema Dk Salehe.

Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya JKCI Alex Benjamini amesema wataalamu wa upasuaji wa kufungua kifua wa JKCI na madaktari Afrika kupitia kambi hiyo wametoa huduma kwa wagonjwa ambao mishipa yao mikubwa ya damu (Aorta) imetanuka, kupasuka au imepata vyote viwili kwa pamoja.

Dk Alex amesema kupitia kambi hiyo wataalamu waamepata fursa ya kuongeza ujuzi na kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya damu kutanuka na kupasuka kutibiwa nchini.

“Matibabu haya ni makubwa na yanahitaji umakini wa hali ya juu, kupitia kambi hii tumepata fursa ya kujifunza na kuongeza ujuzi”, amesema Dk Alex.