Sababu, athari ya ubachela kwenye ndoa

Dar es Salaam. “Kwa takribani miaka mitatu sasa maisha ninayoishi na mume wangu ni kama hatupo ndani ya ndoa. Tunaishi nyumba moja na kulala katika kitanda kimoja lakini kila mtu na maisha yake.

“Sehemu pekee ambayo inatukutanisha na kuzungumza ni katika masuala yanayohusu malezi ya watoto na majukumu ya familia.Mmoja wetu anaweza akapata changamoto na akapambana mwenyewe na kuzitatua bila ya kumshirikisha mwenzake.

Lakini, katika macho ya watu tunaigiza kama watu wenye furaha na ndoa yetu, jambo hili linaniumiza sana na kunifanya kukosa furaha.”

Huyo ni Ramla Ndodi (si jina halisi) akieleza namna ambavyo maisha ya ‘ubachela’ yanavyomtesa ndani ya ndoa yake. Kwake ameolewa kama hajaolewa, kwani anaishi kama alivyokula kabla ya ndoa.

Kinachoelezwa na Ramla kinarandana na  kinachosimuliwa na Joseph Mapunda ambaye yupo katika ndoa kwa takribani miaka mitano sasa, lakini yupo kama hayupo kwani ndoa kwake imekuwa tafrani badala ya ahueni ya maisha.

Anasema maisha ya ndoa kwa miaka miwili ya mwanzo yalikuwa ya furaha lakini baadaye yalibadilika na kuwa mfano wa shubiri.

“Hatuonyeshani mapenzi kama ilivyokuwa awali. Kwa mfano, tunaporudi nyumbani hatuzungumzi zaidi ya salamu, yeye anaangalia tamthilia zake, mimi naingia ‘whatsApp’ au naangalia habari.Hatuna tena muda wa kutembea au hata kula chakula cha jioni pamoja kwa furaha, Sijui kama bado tuna mapenzi, au tuko kwa sababu ya mtoto,” anaeleza.

Kinachosimuliwa na wanandoa hawa ni hali halisi inayotokea katika baadhi ya ndoa katika jamii yetu.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini tabia hii ya maisha ya ubachela ndani ya ndoa, ama kufanywa na mwenza mmoja au wote wawili.

Ukweli ni kuwa mume na mke wanaweza kuishi nyumba moja au hata kulala kitanda kimoja, lakini moyoni wako mbali kama watu wawili waliotengana kwa miaka mingi.

Wengine hutumia sehemu kubwa ya muda wao katika simu, mitandao ya kijamii, maeneo ya burudani,  kazini, vijiweni  au kwa marafiki.

Akizungumza na Mwananchi Pendo John ambaye ni mwanandoa kwa takribani miaka 15,  anasema tabia hiyo kwa wanandoa haitokei ghafla bali husababishwa na changamoto mbalimbali ambazo zinatokea kwenye ndoa na wenza hao kuzifumbia macho

Anatolea mfano wa changamoto hizo kuwa ni pamoja na mawasiliano finyu, kutingwa na majukumu, uwepo wa migogoro ya mara kwa mara ndani ya ndoa pamoja na mabadiliko ya kimwili na kihisia yanayochangia kuwepo kwa hali hiyo kwa wanandoa.

Anasema wanandoa wengi  wanakosa muda wa kuwa pamoja kwa muda mrefu kutokana na kuwa na shughuli nyingi za kujipatia riziki au wakati mwingine  uzembe tu wa  kushindwa kupangilia vizuri ratiba zao za kila siku.

“Kukosa muda wa pamoja kwa wanandoa kwa kufanya mambo yanayowaunganisha kama vile kula chakula pamoja, kuzungumza, kusali pamoja au kutoka matembezini, huchangia ukaribu uliopo kati yao kupungua,”anasema Pendo.

Anaeleza kuwa ukaribu unavyoendelea kupungua hufanya hata mawasiliano baina yao kuwa hafifu.

“Hali hii inaweza kusababisha msongo wa mawazo, uwepo wa migogoro ya mara kwa mara ambayo hatimaye huchochea hali hiyo kutokea,”anasema.

Mtaalamu wa saikolojia, Emelda Mosha anasema changamoto hiyo ipo katika maisha ya baadhi ya wanandoa katika jamii zetu lakini mara nyingi huwa haizungumzwi.

“Mara nyingi wanandoa wanaoishi katika hali hiyo huishi kwa maigizo wanapokutana na watu wengine katika jamii. Huigiza kama wanapendana kumbe ni kinyume chake, ndio maana hili halizungumzwi sana katika jamii,”anaeleza.

Anasema tabia hiyo ya wanandoa kuishi kama hawajaoana  ikiendelea kuota mizizi, inaweza kuleta athari mbalimbali katika ndoa na malezi ya watoto.

Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na migogoro ya mara kwa mara, kupungua au kupotea kwa upendo kwa wenza husika, kuvunjika kwa ndoa, msongo wa mawazo pamoja na usaliti.

“Ukaribu unapopungua, wenza hukosa nafasi ya kushughulikia matatizo kwa pamoja, hali inayoweza kuongeza mivutano na malumbano ya mara kwa mara,anaeleza.

Anaongeza kuwa athari hizo pia huwagusa watoto wanapoona wazazi wao hawana ukaribu na kuwajengea hofu na hata kuwafanya wahisi kutokuwepo kwa upendo nyumbani.

“Asilimia 70 mtoto huelewa na kujifunza kwa haraka kile anachokiona kwa vitendo na asilimia 30 tu ndiyo kwa kusikiliza kile anachoambiwa au kufundishwa,”anasema na kusisitiza kuwa hali hiyo inawaweka watoto katika mazingira magumu ya kimalezi, hasa wanapobaini wazazi hawako pamoja.

Naye mtaalamu wa saikolojia na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Daniel Sendoro, anasema athari nyingine inayoweza kujitokeza ni kuchochea vitendo vya ukatili katika familia.

“Ukatili huo unaweza kuwa wa kipigo, kingono au kisaikolojia hasa kwa wenza wenyewe na wakati mwingine kuwagusa hata  watoto,”anasema.

Sendoro anashauri wanandoa kurudi na kuishi katika misingi ya dini na  viapo vyao vya ndoa.

Pia anasema wanandoa kila mmoja kwa upande wake atekeleze majukumu yake katika ndoa, kutenga muda wa kuwa pamoja, kuboresha mawasiliano kati yao, kuzungumza pale inapotokea changamoto fulani ili kuepuka miogogoro ya mara kwa mara.

Moja, kushuka kwa maadili ya kijamii. Wanandoa wanapochagua kuishi kama mabachela, jamii huanza kupoteza taswira ya ndoa kama taasisi takatifu. Hili linaweza kuhamasisha vijana kuona ndoa kama jambo lisilo na maana, kuchangia ongezeko la uhusiano wa nje ya ndoa, usaliti, na kuvunjika kwa ndoa na hata kupunguza heshima kwa taasisi ya familia katika jamii.

Mbili, changamoto za kiuchumi. Wanandoa wanaoishi kila mtu kivyake,  hulazimika kugharamia maisha kama watu binafsi  kama vile kulipa kodi, chakula, usafiri. Hii huleta mzigo wa kifedha ambao ungeweza kupunguzwa kwa kuishi pamoja.

Zaidi ya hapo huathiri mipango ya kifamilia kama uwekezaji, malezi, na elimu ya watoto na kupunguza ushirikiano wa kiuchumi ndani ya familia.

Wanandoa kuishi kama mabachela ni jambo linaloathiri kwa kiasi kikubwa ustawi na uimara wa familia kama taasisi ya kijamii. Ingawa mazingira mengine huwalazimu kufanya hivyo, ni muhimu jamii kuhamasisha wanandoa kushirikiana maisha kwa karibu, kujenga mawasiliano bora, na kuweka msingi thabiti wa familia kwa ajili ya vizazi vijavyo na jamii kwa ujumla.