Dar es Salaam.Nidhamu ni msingi wa malezi bora na maendeleo ya mtoto, lakini mara nyingi imekuwa ikihusishwa na adhabu kali, vitisho au maneno ya kuumiza.
Ingawa njia hizi zinaweza kutoa matokeo ya haraka, tafiti na uzoefu wa malezi unaonyesha kuwa adhabu kali mara nyingi huacha athari za muda mrefu zinazoweza kuathiri afya ya akili, kujiamini na uhusiano kati ya mzazi na mtoto. Nidhamu chanya inalenga kufundisha, kuongoza na kuhamasisha badala ya kuogopesha au kuadhibu kupita kiasi.
1. Kuelewa Msingi wa Nidhamu Chanya
Lakini ukiyasema haya, wapo watu ambao hutaka kudadisi juu ya hili na kuhoji mambo kadha wa kadhaa.
Lakini tunaambiwa kuwa nidhamu chanya ni mfumo unaojengwa juu ya mawasiliano ya heshima, maelekezo ya wazi na mafunzo yanayojikita katika maadili.
Na hali hii inalenga kuwasaidia watoto kuelewa kwa nini tabia fulani ni nzuri au mbaya na kuwapa nafasi ya kuboresha na msingi wake upo katika uelewa kwamba, watoto wanajifunza vizuri zaidi wanapohisi wapo mahali salama, wanathaminiwa na kusikilizwa na wazazi wao.
Katika hali kama hiyo, wengi wao wenye kufuata haya niliyoaandika hapoa juu, huwafanya wajifunze kwa kuiga kusudi nao waje kuwa mfano bora kwa watoto wao.
Mtaalamu wa saikolojia Gabriel Mwakipesile aliwahi kuniambia kuwa mzazi au mlezi anayezungumza kwa heshima, kushughulikia changamoto kwa utulivu na kushirikiana kwa upendo na watoto wake, hutazamwa na wanawe kuwa mfano wa moja kwa moja wa nidhamu.
Badala ya kuhubiri tu, mzazi huyo anapaswa kuonyesha kwa vitendo hali hiyo kama kushukuru, kuomba radhi anapokosea na kuheshimu utaratibu waliojiwekea nyumbani. Anasema tabia za mzazi mara nyingi huwa “darasa la kwanza” la mtoto. Tafakari niliyojifunza katika hili inanielekeza kuwa;
watoto hujitahidi kurudia tabia zinazotambulika kama nzuri visifa vidogo kama vya mzazi kumpa hongera mwanawe pale anapokuwa amefuata maelekezo sahihi aliyompatia.
Anaweza kumwambia mtoto pia “nimefurahi ulipomaliza kazi yako mapema,” hali hii humfurahisha na anaweza kuongeza ari ya kufanya vizuri zaidi.
Watoto wanahitaji kuelewa kwa uwazi misimamo au makatazo ya familia na sababu zake.
Misimamo isipoelezwa, adhabu yoyote inaweza kuonekana kama unyanyasaji dhidi yake. Kwa mfano, badala ya kusema “usiwe unapiga kelele hovyo wakati tunakula chakula,” basi mzazi amwambie mwanawe; “Tunapokuwa mezani tunazungumza kwa sauti ya chini ili kila mtu asikie vizuri.” Maelezo kama haya humsaidia mtoto kujua kumbe alichokuwa akikifanya si sahihi na kinawakwaza wengine.
Sasa wapo wazazi badala ya kufanya hivyo, wao huwapa adhabu kali watoto wao kwa kosa kama hilo na matokeo yake, hujenga visasi au malipizi kwa watoto.
Tukumbuke watoto wanapohisi wanasikilizwa, mara nyingi hupunguza ubishipinzani na kuongeza ushirikiano.
Mazungumzo ya utulivu yanayojumuisha maswali kama “Unadhani ungeweza kufanya nini tofauti?” humfanya mtoto kushiriki katika kutafuta suluhisho badala ya kuhisi anashinikizwa. Hii pia hujenga stadi za kufikiria kwa kina na kutatua matatizo.
Ndiyo maana wataalam wa malezi husisitiza kwamba, kumwelekeza mtoto njia sahihi ya kuamua mambo, humsaidia kujifunza uwajibikaji na kufanya uamuzi.
Badala ya kusema “safisha chumba chako sasa hivi,” unaweza kusema “ungependa kuanza na vitabu au nguo?” Uchaguzi huondoa hisia ya kulazimishwa na hujenga tabia ya kupanga kazi.
Utaratibu wa kila siku ndani ya familia, hujenga nidhamu kwa watoto. Mfano wakati wa kula, kusoma na kulala unapowekwa wazi, mtoto anatambua jukumu lake hivyo hmusaidia kupunguza migongano ya kila siku.
Utaratibu pia hujenga hisia ya usalama na uthabiti, mambo muhimu kwa ukuaji wa kihisia.
Hata hivyo, mabadiliko ya tabia hayaji mara moja. Nidhamu chanya inahitaji uvumilivu, msimamo na mzazi kurudia kumwelekeza kwa upole.
Mara mtoto anapojua kwamba utaratibu ni uleule kila wakati na hauna mabadiliko ya ghafla, atajenga imani na kujifunza kuendana nao na kuuzingatia.
Mara nyingine, mzazi au mlezi anapaswa kujiuliza: “Je, ninachokifanya kinamfundisha mtoto au kinamwumiza?”
Shadya Mbaga, mtaalamu wa malezi anasema kitendo cha mzazi kujitathmini, husaidia kutambua maeneo ya kuboresha.
Tukumbuke kuwa lengo la nidhamu si kushinda hoja, bali kufundisha maadili na stadi za maisha kwa mtoto.
Nidhamu chanya si kulegeza masharti au kumwachia mtoto bila mwongozo. Bali ni njia yenye malengo na maadili, inayolenga kuwajenga watoto wanaojitambua, wenye heshima na wanaowajibika.
Kupitia mfano bora yanamfanya mzazi aonekane mbele ya jamii kwamba anasimamia nidhamu imara bila kutumia adhabu kali kwa wanawe.
Hii si tu njia ya kulea watoto bora, bali pia hujenga familia yenye mshikamano, heshima na upendo wa kudumu.