Dar es Salaam. Baada ya kuhudumu kwa miaka 15 akiwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla amewaaga wananchi wa Nzega akiwataka kutoa ushirikiano kwa mwakilishi wao mpya.
Dk Kigwangalla ni miongoni mwa waliokuwa wabunge kwenye Bunge la 12 ambao michakato ya ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imewaweka kando kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Baada ya michakato mirefu ya ndani ya kuwapata wagombea, usiku wa jana Jumamosi, Agosti 23, 2025 ilitangaza walioteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho, huku Dk Kigwangalla akiwa si sehemu yao.
Katika kura za maoni, Dk Kigwangalla aliishia nafasi ya pili kwenye kura za maoni akipata kura 1,715 dhidi ya mshindani wake, Neto Kapalata aliyepata kura 2,570.
Safari ya kuongoza Jimbo la Nzega Vijijini kwa awamu nyingine sasa itakuwa chini ya Neto Kapalata ambaye Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) katika kikao chake cha Agosti 23, 2025 imemteua kukiwakilisha chama hicho.
Kufuatia hatua hiyo, Dk Kigwangalla katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram ameandika ujumbe wenye maudhui ya kuwaaga wananchi wa Nzenga aliowatumikia kwa miaka 15. Mwaka 2010 alianza akiwa mbunge wa Nzenga.
Mwaka 2015 lilipogawanywa na kuwa majimbo mawili Nzega Mjini na Nzega Vijijini, yeye alikwenda Nzega Vijijini huku Hussein Bashe akiwa Nzega Mjini.
Miaka 15 akiwa mbunge, Dk Kigwangalla alifanikiwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Waziri wa Maliasili na Utalii.
Katika maelezo yake kwa wananchi wa Nzega, Dk Kigwangalla ameandika; Kwa miaka 15 tumetembea pamoja. Tumeshirikiana kujenga Nzega mpya inayoonekana na kupendeza leo, tumeshirikiana katika changamoto, na tumeshirikiana katika ndoto ya kuliletea jimbo letu heshima na nafasi yake stahiki. Safari ya kura za maoni imehitimishwa, na safari hii haikuwa yetu.
Nimepokea matokeo haya kwa moyo wa unyenyekevu, nikitambua kwamba demokrasia ndani ya chama chetu ni nguzo kuu ya uimara wake.
Alhamdulillah kwa kunifikisha hatua hii. Nawashukuru kwa dhati wananchi wote wa Jimbo la Nzega (nilipohudumu miaka 5) na wa Nzega Vijijini (nilipohudumu miaka 10), kwa imani, upendo na mshikamano mlionipa kwa kipindi chote cha utumishi wangu. Ni heshima kubwa kwangu kuwawakilisha na kuwatumikia kwa kipindi cha miaka 15.”
“Kwa heshima ya kipekee, namshukuru sana Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti, hekima yake ya kipekee, na dhamira yake njema ya kuliongoza Taifa letu na chama chetu kwa uadilifu, mshikamano na mafanikio makubwa.
Mimi nitaendelea kuwa askari mwaminifu chini ya uongozi wake, nikiwa tayari kulitumikia Taifa langu na chama changu popote nitakapohitajika.
“Tumpokee kwa heshima aliyeteuliwa, tumtie moyo na tushirikiane naye kuendeleza kazi ya kuwatumikia wananchi. Mimi nitaendelea kuwa mwana-CCM mwaminifu na Mtanzania mtiifu.
“Mungu ibariki Nzega Vijijini, kidumu Chama Cha Mapinduzi, na Mungu ibariki Tanzania,”ameandika Kigwangalla.
Huyu ndiye Dk Kingwangalla
Dk Kigwangala alizaliwa Agosti 7, 1975 mkoani Kigoma, alisoma Shule ya Msingi Kitongo-Nzega, Sima –Bariadi na kumaliza Mwanzoli-Nzega.
Elimu ya upili, alisoma Shule ya Sekondari Kigoma kidato cha kwanza mpaka cha nne na baadaye alijiunga kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Shinyanga (Shy Bush) akichukua mchepuo wa PCB (Physics, Chemistry, Biology).
Mwaka 1999 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alichukua masomo ya udaktari wa binadamu na alihitimu shahada yake mwaka 2004.
Alichaguliwa kuwa mbunge wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 1999 na baadaye Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu, Mwaka 2000.
Dk Kigwangalla vilevile amepata Shahada ya pili kwenye Afya ya Jamii (Masters of Public Health, MPH) amebobea zaidi kwenye Utafiti wa Mifumo ya Sekta ya Afya na kuhamasisha usalama, kutoka Chuo Kikuu Cha Karolinska, jijini Stockholm, Sweden (2006).
Pia alipata shahada nyingine kwenye Biashara na Utawala (Masters of Business Administration, MBA) amebobea zaidi kwenye uongozi, oganaizesheni, mikakati ya maendeleo na masoko, kutoka Chuo Kikuu Cha Blekinge, Mjini Ronneby/Karlskrona, Sweden (2007).
Kigwangalla aliingia katika orodha ya watangaza nia ya urais ndani ya CCM zaidi ya 35 katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Septemba 7, 2014 jijini Dar es Salaam lakini jina lake halikupenya.