Samia amjengea nyumba Bibi Catherine na wajukuu zake sita

Bukoba. Serikali imemkabidhi nyumba mpya Catherine Nathahiel pamoja na wajukuu zake sita, baada ya kupoteza makazi yao kufuatia mafuriko yaliyoikumba Manispaa ya Bukoba, Mei 10, 2024.

Nyumba hiyo imejengwa kwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kama sehemu ya ahadi yake ya kuwasaidia waathirika wa maafa hayo.

Mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo, yalisababisha Mto Kanoni kufurika na kuharibu makazi ya wananchi katika kata za Nshambya na Bilele.

Miongoni mwa walioathirika ni familia ya bibi Catherine, aliyekuwa mkazi wa Mtaa wa Migera, Kata ya Nshambya, ambaye nyumba yake iliporomoka na kusombwa na maji.

Akizungumza leo Jumapili, Agosti 24, 2025, wakati wa makabidhiano ya nyumba hiyo yenye vyumba vitatu, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema ujenzi na ununuzi wa kiwanja vimegharamiwa na Serikali kwa maagizo ya Rais Samia.

“Baada ya kukagua athari za mafuriko, tulibaini familia hii yenye wajukuu sita ilipoteza kila kitu. Mara ya kwanza tuliwasaidia chakula na vifaa vya shule na tulipowasilisha taarifa kwa Rais Samia, alielekeza familia hii ipatiwe makazi ya kudumu ili watoto wasipelekwe kwenye vituo vya kulelea yatima,” amesema Mwassa.

Mkuu wa mkoa Kagera, Fatma Mwassa akiwa na wajukuu wa bibi huyo.



Nyumba hiyo imejengwa katika kiwanja kilichopimwa na Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na kupewa hati namba 102, kilichopo kitaru F, Kata ya Buhembe.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amesema familia ya bibi Catherine imekuwa ikiishi kwa hifadhi ya mtumishi wa idara ya afya, Adelina Wilson, ambaye aliwapokea tangu walipopata madhila ya mafuriko.

“Adelina aligundua familia hii haina msaada, akawakaribisha nyumbani kwake na kutuomba waendelee kuishi naye. Kupitia msaada wake na vyombo vya habari, Serikali ilipata taarifa za changamoto wanazopitia,” amesema Sima.

Kwa upande wake, bibi Catherine ameishukuru Serikali na Rais Samia kwa kuwapatia makazi salama, akisema sasa anaweza kuwatunza wajukuu zake kwa amani.

“Nashukuru sana kwa kutuweka tena kwenye nyumba salama. Nimekuwa nikiishi na wajukuu hawa kwa sababu walipoteza wazazi wao wote, na mimi pia nimefiwa na watoto wangu watatu ambao walikuwa wazazi wao,” amesema bibi Catherine.

Miongoni mwa wajukuu hao, Loveness Matungwa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Hamugembe, amesema wamepokea nyumba hiyo kama muujiza.

“Tangu tuwapoteze wazazi wetu, hatukutegemea kama siku moja tutalala sehemu salama kama hii. Tunashukuru sana kwa nyumba hii mpya,” amesema Loveness.