Sura mbili waume kuwazuia wake kufanya kazi

Dodoma. Juzi nilikutana na mjadala mkali nisioutarajia maeneo ya Posta jijini Dar.

Nilikuwa nikisafisha viatu katika kijiwe kimoja kinachowakutanisha watu wengi wanaopenda kujadili masuala kadhaa wakisubiri huduma hiyo.

Mjadala wenyewe ulianzishwa na mzee mmoja, mtumishi wa umma, anayeonekana kukaribia kustaafu. Mzee alimlalamikia mkwe wake kwa kumnyanyasa mwanawe.

Hakuonekana kumfahamu yeyote kati yetu pale kijiweni hali inayotafsirika kama kuzidiwa na jambo hilo lililomnyima amani.

“Nimemsomesha mtoto wangu wa kike kwa mbinde. Nimehangaika hasa kuhakikisha anasoma kama wenzake wa kiume. Sikuwa na maisha na mpaka leo hapa tunavyoongea sina hata chumba nilichojenga lakini nilifunga mkanda mwanangu apate taaluma,” alisema.

Masuala haya, kwa kawaida, ni vigumu kuyasikia yakijadiliwa hadharani. Nilitafsiri kama ishara njema kuwa mzee huyu, kwani  alitambua umuhimu wa kusema yanayomsibu bila woga.

“Mtoto ana uwezo mkubwa na alifaulu vizuri chuo kikuu na tayari alikuwa anafanya kazi. Imepita miaka miwili katuambia anaolewa tukafurahi. Tumemuoza. Kituko mume hataki mke wake afanye kazi. Kamwachisha kazi.”

Simulizi ya mzee inaonesha kijana aliyemuoa binti yake alifanya mbinu kuhakikisha hawezi tena kuendelea na kazi. Ilibidi tu aache kazi.

“Kijana ana kazi ya kawaida. Hana kipato kikubwa na maisha wanayoishi ni kama yangu. Inaniuma kuona mtoto anazuiwa kufanya kazi wakati wangeweza kusaidiana kuendesha maisha,”alisema na kuongeza:

“Hebu nishaurini nifanyaje? Kumwachia huyu mtu aamue anavyotaka ni sawa? Hata kama ana uwezo wa kutunza familia na mambo ya ndoa ni ya watu wawili, mimi niliyemsomesha mtoto sitakiwi kusema chochote ninapoona mwanangu anageuzwa kuwa mama wa nyumbani? Nikisema ninakuwa naingia ndoa ya watu?”

Mjadala ulikuwa na pande mbili. Upande wa kwanza uliunga mkono msimamo wa kijana kumwachisha kazi mke wake ukisisitiza wazazi kutoingilia uamuzi wa watoto wao. Hoja kubwa iliyoubeba upande huu ni wajibu wa kimaumbile wa mwanamke katika malezi.

“Heshima ya mwanamke haipo kwenye vyeo na kipato anachopata kazini. Heshima ya mwanamke ni namna anavyowalea watoto. Kwa hiyo huyo kijana amefanya uamuzi sahihi,” alisema mchangiaji mmoja.

Hoja ya pili ilijikita kwenye ‘kiburi’ cha wanawake wanapokuwa na kipato. “Hawa wanawake wakiwa na uwezo wanakuwa tatizo kwenye ndoa.

Kule kazini wanakutana na watu tofauti na tunajua ndoa nyingi zinasalitiwa ofisini. Ukijumlisha na uwezo wa kifedha unajikuta huna chako.”

Hata hivyo,  upande wa pili ulisimama na mzee kuhoji uhalali wa mwanamume kuzima ndoto za mwanamke.

“Kama ilivyo kwa mwanamume, mwanamke naye ana ndoto na matamanio katika maisha. Huwezi kutumia hoja hizi dhaifu kugeuza jitihada zote zilizofanywa na wazazi zionekane hazina maana. Kama alikuwa anataka mwanamke wa kulea watoto angeenda kutafuta darasa la saba waje wafanye kazi hiyo. Kumgeuza mwanamke msomi kuwa mama wa nyumbani ni jambo lisilokubalika hata kidogo.”

Hoja hii ilipingwa na mchangiaji aliyefikiri msemaji wa mwisho katika familia ni mwanaume.

“Nani ni kichwa cha familia? Kwa nini tunataka kuingilia uamuzi halali wa mume? Hata kama mwanamke hataki jambo, mwanamume akishasema ndio inakuwa hivyo,” alisema mshiriki mwuingine.

Kufikia hapo ilianza kuonekana wazi kuwa msimamo wa kumzuia mwanamke kufanya kazi sawa na mwanamume una mizizi yake kwenye mfumo dume.

Fikra kwamba mwanamke anaweza kusoma na akaachana na ndoto zake kwa amri ya mwanamume zinaonesha kuwa bado tuna safari ndefu linapokuja suala la usawa wa kijinsia kwa maana ya mwanamume na mwanamke kuwa na hadhi sawa ya kuishi maisha yenye staha kutimiza ndoto zao.

Suala la ipi ni mipaka ya wazazi kufuatilia maisha ya watoto wao hata baada ya ndoa nalo likajitokeza. Pamoja na umuhimu wa mzazi kuwaacha watoto wake kuishi maisha yao, tunaweza vipi kupuuza hisia zake anaposikia kuna jambo haliendi sawa kwenye ndoa ya mwanawe?

Tunaheshimu vipi rasilimali nyingi alizotumia, muda, mali na fedha, kuhakikisha mtoto anasoma? Hiki ndicho hasa kinachomtesa mzee wetu.

 Umuzi wa mume wa binti yake unaonekana kupuuza kabisa jitihada zake za kuhakikisha binti yake anaishi maisha ya staha.

Maneno kama, “Mzazi hamsomeshi mtoto kwa matarajio ya kuja kusaidiwa baadaye” yanaweza kuonekana yana hekima kubwa yasipofikiriwa vizuri.

Unapotaka mzazi aliyepambana, wakati mwingine kufa na kupona, ajiweke pembeni, asiingilie maisha ya mwanawe, asimsumbue kwa lolote, unakuwa umefikiri sawa sawa?

Hata kama ni kweli mzazi anaweza kuwa na matarajio na binti yake, hilo linakuwaje kosa? Kwamba mzazi ajinyime, avae shati moja, akope, auze ng’ombe, auze mashamba, akupeleke shule lakini ukishapata maisha yako unamwambia tu kirahisi, “Ulifanya wajibu wako usitarajie chochote kwangu?”

Mazingira gani yanamfanya mzazi kuingilia maisha ya ndoa ya mwanawe? Nitaanzia hapa wiki ijayo.