Wasaini kanuni za maadili wakikumbushwa kuzingatia wajibu

Unguja. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi, amezitaka pande tatu zinazohusika katika mchakato wa uchaguzi kuzingatia maelekezo ya kanuni za maadili ili kuhakikisha uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, unafanyika kwa amani, haki na mshikamano.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Agosti 24, 2025, katika ofisi kuu za ZEC Maisara, wakati wa hafla ya kusaini kanuni za maadili ambazo zitatumika katika kipindi chote cha uchaguzi.

Kanuni hizo zimesainiwa na vyama vya siasa, ZEC na mamlaka za Serikali. Vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu vimesaini kanuni hizo, isipokuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho hakukuwa na mwakilishi wake.

Jaji Kazi amesema kifungu cha 65 cha Sheria ya Uchaguzi Namba 4 ya mwaka 2018 kinaitaka tume kushirikiana na vyama vya siasa, Msajili wa Vyama na mamlaka za Serikali kutayarisha kanuni za maadili zitakazoongoza wadau katika shughuli za uchaguzi.

“Pande zote tatu zinazotia saini leo lazima zitekeleze wajibu wao kama inavyobainishwa na kanuni hizi. Lengo ni kuwa na uchaguzi wa kihistoria, wa kidemokrasia na wa kuaminika kwa wananchi,” amesema Jaji Kazi.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, vyama vya siasa vinatakiwa kulinda usalama, amani na haki za makundi yote, kuheshimu wagombea wakiwamo wanawake na watu wenye ulemavu, kutoshiriki matusi au uchochezi na kuzingatia muda wa kampeni.

Kwa upande wa tume, wajibu wake ni kuhakikisha inafuata Katiba na sheria, kutoshabikia chama au mgombea yeyote, kushughulikia malalamiko kwa uadilifu na kutoa taarifa kwa uwazi.

Serikali imetajwa pia kuwa na jukumu la kutoa huduma sawa kwa vyama vyote, kuchukua hatua za kisheria kwa viongozi watakaovuruga kanuni na kuhakikisha vyombo vya usalama vinatoa ulinzi bila upendeleo. Pia imekatazwa matumizi ya mali za Serikali kwa shughuli za kisiasa.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa ZEC ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Jaji Aziza Iddi Suweid, amesema lengo la kanuni hizo ni kuhakikisha usawa na uchaguzi wa amani kwa kuzingatia haki na vigezo vya kikanda na kimataifa.

Kamati ya maadili inaundwa na wawakilishi wa ZEC, vyama vya siasa vyenye usajili, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca), Ofisi ya Rais Tamisemi na Sekretarieti ya ZEC.

Wakizungumza baada ya kusaini, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamesisitiza umuhimu wa kutekeleza kanuni hizo badala ya kuziacha kuwa maandiko pekee.

Mwanasheria Mkuu wa ACT-Wazalendo, Omar Said Shaaban, amesema changamoto iliyopo ni kutowekwa adhabu kwa watendaji wa tume na Serikali watakaokiuka kanuni.

“Tukitekeleza wajibu wetu, uchaguzi wa haki na huru utapatikana, lakini vyombo vya Serikali pia vinapaswa kuwajibishwa,” amesema.

Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya CCM Zanzibar, Omar Ibrahim Kilupi, amesema chama chake kimejipanga kulinda amani.

“Bila amani hakuna uchumi. Tutahakikisha kampeni zetu hazimkwazi mtu na tunakwenda pamoja kuchagua viongozi wetu,” amesema Kilupi.

Katibu Mkuu wa chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir, akizungumzia hilo, amesema: “Kuna maisha baada ya uchaguzi. Tunataka watu wanadi sera, chama kitakachokubalika ndicho kitakachoongoza bila vurugu.”

Naye Mwenyekiti wa AAFP, Said Soud Said, kwa upande wake amesema chama chake kinaingia kwenye uchaguzi kwa nia ya maendeleo, si kuvuruga amani.

Kabla ya kusaini kanuni hizo za maadili, wadau hao wameshiriki matembezi ya amani kutoka ukumbi wa Abduwakili Kikwajuni hadi ofisi kuu za tume, ambako kumezinduliwa rasmi nembo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.